WAZIRI ULEGA AIPONGEZA TTCL KWA KUCHOCHEA MAGEUZI YA KIDIJITALI KUPITIA HUDUMA ZA MAWASILIANO
Na Debora Ngalima
Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Abdallah Ulega (Mb), amelipongeza Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kwa kuendelea kuwekeza katika huduma za mawasiliano zinazochochea mageuzi ya kidijitali na kurahisisha upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa wananchi na Taasisi nchini.
Waziri Ulega alitoa pongezi hizo leo baada ya kutembelea banda la TTCL katika Mkutano wa 23 wa Wahandisi unaofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, mkutano unaowakutanisha zaidi ya wahandisi 4,000 kutoka taasisi za Serikali na sekta binafsi.
Katika ziara hiyo, Waziri alipata fursa ya kufahamu huduma na suluhisho mbalimbali za kiteknolojia zinazotolewa na TTCL, ikiwemo mchango wa Shirika hilo katika kujenga mazingira bora ya mawasiliano yanayowezesha taasisi, wafanyabiashara na wananchi kutumia fursa za uchumi wa kidijitali.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Waziri Ulega alisisitiza umuhimu wa ubunifu na matumizi ya teknolojia katika kuendeleza sekta mbalimbali, huku akitambua jitihada zinazofanywa na wadau wa mawasiliano katika kuimarisha miundombinu ya kidijitali nchini.
Kwa upande wake, TTCL imeendelea kuonyesha dhamira yake ya kuwa mshirika wa maendeleo kwa kuhakikisha wananchi na taasisi wanapata huduma za mawasiliano zenye ubora, zinazosaidia kuongeza tija, kukuza biashara na kufungua fursa mpya katika uchumi wa kisasa.
Ushiriki wa TTCL katika mkutano huo unaonyesha nafasi ya sekta ya mawasiliano kama kichocheo muhimu cha maendeleo ya Taifa, ambapo huduma bora za intaneti na mifumo ya kidijitali zinaendelea kusaidia kuongeza ufanisi katika biashara, elimu, huduma za umma na shughuli mbalimbali za kijamii.
Mkutano wa 23 wa Wahandisi unafanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 24 hadi 25 Septemba 2026, umebeba kaulimbiu “Kukuza Ubunifu wa Uhandisi na Mageuzi ya Kidijitali kwa Maendeleo Endelevu”.