info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

WAZIRI SIMBACHAWENE APONGEZA TTCL KWA HUDUMA BORA NA UWEKEZAJI WA KISASA

Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limeendelea kudhihirisha dhamira yake ya kuimarisha mawasiliano nchini kwa kuonesha teknojia ya kisasa wakati wa Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma mwaka huu 2025 yanayofanyika katika Viwanja vya Chinangali, jijini Dodoma.

Maadhimisho haya yamefunguliwa rasmi June 16 mwaka huu, huku Mgeni Rasmi wa Maonesho hayo akiwa ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (Mb).

Mhe. Simbachawene pamoja na mambo mengine ametembelea banda la TTCL na kupata fursa ya kukutana na Maafisa wa shirika hilo na kujionea huduma na bidhaa mbalimbali zinazotolewa kwa wananchi katika kukuza matumizi ya TEHAMA nchini.

Waziri Simbachawene amelipongeza Shirika hilo kwa mchango wake mkubwa katika sekta ya mawasiliano, hususan kwa kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi na kuwekeza katika teknolojia za kisasa. 

“Mawasiliano ni mhimili wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi ni muhimu kwa mafanikio ya Taifa letu,” alisisitiza Waziri Simbachawene.

Katika maonesho hayo TTCL imewasilisha huduma bunifu na muhimu zikiwemo huduma za simu, intaneti ya kasi, huduma za kifedha kupitia simu, Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na kituo cha kuhifadhi Data (NIDC) na hivyo Wananchi walipata nafasi ya kujengewa uelewa wa mawasiliano, kufahamu teknolojia mpya na kujisajili moja kwa moja kwenye huduma mbalimbali zinazotolewa na shirika hilo.

Kupitia kaulimbiu ya mwaka huu, “Himiza Matumizi ya Mifumo ya Kidijitali ili kuongeza upatikanaji wa taarifa na kuchangia uwajibikaji”, TTCL imeonesha namna miundombinu yake, hasa huduma ya intaneti ya kasi kupitia teknolojia ya Faiba, inavyowezesha utekelezaji wa mfumo wa Serikali Mtandao (e-Government) katika Taasisi za Umma nchini.

Ushiriki wa TTCL katika maonesho haya umelenga si tu kuelimisha wananchi kuhusu huduma zake, bali pia kuimarisha matumizi ya teknolojia katika sekta ya umma kwa lengo la kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi wa utoaji huduma kwa jamii.

.