info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

WAZIRI SILAA AZINDUA MNARA WA TTCL KIJIJI CHA HIKA WILAYA YA MANYONI SINGIDA

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Jerry Silaa (Mb) amezindua rasmi mnara wa mawasiliano wa TTCL katika Kijiji cha Hika, Wilaya ya Manyoni, Mkoa wa Singida.

Uzinduzi huu ni sehemu ya juhudi za Serikali kupitia Shirika hilo za kuimarisha upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa wananchi wa vijijini, ikiwa ni pamoja na kufikisha huduma za simu na intaneti maeneo ambayo awali yalikuwa na changamoto ya mawasiliano.

Kupitia mnara huo, wananchi wa Kijiji cha Hika na maeneo jirani wataweza kunufaika na huduma za mawasiliano za TTCL, hatua inayolenga kuboresha shughuli za kiuchumi, kijamii, na maendeleo ya kijamii kwa ujumla. 

TTCL kwakushirikiana na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) inaendelea na mpango wa kupanua mtandao wake wa mawasiliano ili kuwafikia watanzania wengi zaidi katika maeneo ya vijijini na mijini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Waziri Silaa alilipongeza shirika hilo pamoja na Viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Singida kwa ushirikiano wanaounesha katika kuwaletea maendeleo Wananchi hasa wa Kijiji cha Hika ambacho kabla ya ujenzi wa mnara huo hakikuwa na mawasiliano yoyote ya mtandao wa simu.

Akisoma taarifa ya mradi huo Meneja wa TTCL Mkoa wa Singida Bw. Agustino Mwakyembe alisema kukamilika kwa mnara huo ni utekelezaji wa dhamira ya Serikali kupitia Shirika hilo kuimarisha Hali ya mawasiliano vijijini ambapo shirika limekuwa likifanya maboresho ya minara ya mawasiliano kutoka Teknolojia ya 2G hadi 4G. 

Bw. Mwakyembe alisema kuanzishwa kwa Mawasiliano ya Teknolojia ya 4G katika maeneo ya vijijini ikiwemo Hika kinatarajiwa kuleta mapinsuzi makubwa katika matumizi ya TEHAMA na huduma za kijamii kupatikana kidigitali. 

Alisema mnara huo uliozinduliwa utahudumia jumla ya vijiji vitatu vya Hika, Londoni na Msemembo vyenye jumla ya wakazi zaidi ya elfu ishirini na nne.