WAZIRI SILAA ATEMEBELEA KITUO CHA MKONGO ITIGI SINGIDA
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Jerry Silaa Oktoba 22 Mwaka huu, alitembelea kituo cha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kilichopo Wilaya ya Itigi mkoani Singida.
Waziri Silaa alitembelea kituo hicho ikiwa ni ziara yake ya siku tano mkoani humo lengo likiwa ni kufuatilia, kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na mradi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ambao unakusudia kuboresha upatikanaji wa huduma za mawasiliano nchini kote.
Akiwa kituoni hapo Mhe. Waziri alipata maelezo kuhusu mradi huo kutoka kwa Meneja wa TTCL Mkoa wa Singida Bw. Agustino Mwakyembe ambapo alimweleza kuwa kukamilika kwa kituo hicho kumeongeza ubora wa upatikanaji wa huduma za Mawasiliano na Intaneti katika taasisi za kifedha, Mashirika yaserikali na yasiyo ya kiserikali yaliyopo katika Wilaya hiyo na maeneo jirani.
Alisema shirika linatarajia mradi huo utatoa chachu ya upatikanaji wa huduma ya mawasiliano katika mikoa ya Singida, Tabora na Mbaya na kussidia kukuza uchumi wa kidigitali.
Katika ziara hiyo, Waziri Silaa alisisitiza umuhimu wa miundombinu hii kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii, huku akitoa wito kwa wadau kuunga mkono juhudi za serikali za kuhakikisha kila Mtanzania anafaidika na fursa za kidijitali zinazoletwa na mkongo huo.