info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

WAZIRI MKUU MAJALIWA AFUNGA RASMI KONGAMANO LA TEHAMA 2024

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) amefunga rasmi Kongamano la 8 la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) la mwaka 2024 lililofanyika kwa siku tano katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam. 

Kongamano hilo, lililofanyika likiwa na kaulimbiu ya “kutumia Uwezo wa Akili Mnemba na Robotiki kwa Mapinduzi ya Uchumi na Kijamii” iliyolenga kuhimiza maendeleo ya uchumi wa kidigitali hapa nchini, liliwaleta pamoja wataalamu wa teknolojia, wadau wa sekta ya mawasiliano, wajasiriamali, na wafanyabiashara kutoka ndani na nje ya nchi.

Shirika la Mawasiliano Tanzania katika kongamano hili lilikuwa ni mdau mkubwa kutokana na usimamizi na uendeshaji wa miundombinu ya mawasiliano ambayo imesambaa nchi nzima ambayo imechangia katika kukuza matumizi ya TEHAMA. 

Uwepo wa miundombinu ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano- NICTBB na Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Data Kimtandao- NIDC vimechangia katika kuimarisha matumizi ya TEHAMA nchini ambayo ndiyo ilikuwa shabaha kubwa katika kongamano la mwaka huu 2024. 

Katika Kongamano hilo, TTCL ilidhamini huduma ya intaneti –Wi Fi ikiwa ni mkakati wa Shirika hilo katika kuhakikisha Mikutano mikubwa ya Kitaifa na Kimataifa inakuwa na huduma bora ya Intaneti yenye kasi na uhakika.

Kongamano hili limekuwa fursa muhimu ya kubadilishana mawazo na mbinu bora za kuendeleza teknolojia ya kidigitali nchini, ikiwemo kutoa majibu kwa changamoto zinazokabili sekta hiyo kama vile usalama wa mitandao na upatikanaji wa huduma za mtandao kwa wote.