info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

WAZIRI MKUU AKABIDHI TTCL TUZO YA NAFASI YA TATU KATIKA SEKTA YA MAWASILIANO – MAONESHO YA 49 YA SABASABA

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) amekabidhi tuzo ya nafasi ya Tatu katika Sekta ya Mawasiliano kwa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) wakati wa kilele cha Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (SabaSaba), ikiwa ni kutambua mchango na ubunifu wa Shirika hilo katika utoaji wa huduma bora za mawasiliano nchini.

Tuzo hiyo ya heshima imepokelewa kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Bw. Moremi Marwa, na Mkurugenzi wa Ufundi, Bw. Cecil Francis, katika hafla iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, sekta binafsi na washiriki wa maonesho hayo.

Maonesho ya mwaka huu yaliyoongozwa na kaulimbiu ya Maonesho ya Biashara ya Kimataifa (SabaSaba) Fahari ya Tanzania, yametoa jukwaa kwa TTCL kuonesha uwezo wake mkubwa wa kiteknolojia, zikiwemo huduma za intaneti ya kasi, suluhisho kwa taasisi na biashara, huduma za simu, pamoja na huduma za kifedha kupitia T-Pesa.

Ushindi huu, unadhihirisha kuwa TTCL inaendelea kuonesha nafasi yake katika safari ya mabadiliko ya kidijitali nchini, huku Shirika hilo likiwa na dhamira ya kutoa huduma salama, thabiti na za kuaminika kwa maendeleo ya taifa.

Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo Bw. Cecil Francis kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu –TTCL, ametoa pongezi za dhati kwa timu ya mauzo ya Shirika hilo kwa kazi nzuri waliyoifanya katika kipindi chote cha maonesho hayo kwa kuonesha weledi, ubunifu na kujituma kwao, hatua iliyochangia mafanikio haya makubwa.

Ushindi huu ni mafanikio ya TTCL katika kuendelea kuwa chachu ya mapinduzi ya kidijitali, kuweka msingi imara wa Tanzania ya kidijitali na yenye ushindani katika soko la Kikanda na Kimataifa.

.