info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

WAZIRI KAPINGA AIPONGEZA TTCL KWA FAIDA NA GAWIO KWA SERIKALI

WAZIRI wa Viwanda na Biashara Mhe. Judith Kapinga, ameipongeza Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kwa kuendelea kufanya vizuri kibiashara, kupata faida, kutoa gawio kwa Serikali pamoja na kutunukiwa tuzo maalum na Rais Samia Suluhu Hassan.

Kapinga ameyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati alipotembelea banda la TTCL lililopo kwenye Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa maarufu sabasaba ambapo amesema mafanikio hayo yanaonesha kuwa TTCL imeendelea kuimarika na kuwa taasisi yenye mchango mkubwa katika maendeleo ya sekta ya mawasiliano na uchumi wa taifa.

Amesema hatua ya shirika hilo kupata faida na kurejesha gawio serikalini ni ishara ya usimamizi mzuri wa rasilimali za umma na utekelezaji wenye tija wa mikakati ya biashara.

Aidha, amesema TTCL inaendelea kukua kwa kasi na kuwa mhimili muhimu katika kuhamasisha uchumi wa kidigitali nchini kupitia uwekezaji katika miundombinu ya mawasiliano, hususan huduma za mkongo wa taifa na teknolojia za kisasa.

Kwa upande wake Ofisa Uhusiano kwa TTCL, Emerco Mashelle amemweleza waziri kuwa uwekezaji katika viwanda vya ndani vya kutengeneza fibre utapunguza kwa kiasi kikubwa gharama za ununuzi wa vifaa kutoka nje ya nchi, hatua itakayowezesha TTCL kuwafikia wateja wengi zaidi nchini.

“Tunawajengea wateja huduma ya fibre bure hadi mlangoni mwao. Uwepo wa viwanda hivi hapa nchini utatusaidia kupata vifaa kwa gharama nafuu, jambo litakalotuwezesha kupanua mtandao na kuwafikia wananchi wengi zaidi,” amesema.

Amesisitiza kuwa upatikanaji wa vifaa vya mawasiliano vinavyozalishwa nchini ni hatua muhimu katika kuimarisha sekta ya mawasiliano na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wananchi.