info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

WAZIRI KAIRUKI AITAKA TTCL KUONGEZA UWEKEZAJI ILI KUIMARISHA USHINDANI NA KUCHOCHEA UCHUMI WA KIDIJITALI

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Kairuki (Mb), ameuelekeza uongozi wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kuongeza uwekezaji katika maeneo ya kimkakati, ikiwemo mradi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB), huduma ya FTTH, pamoja na Kituo cha Kuhifadhi Data Kimtandao (NIDC), ili kuongeza ushindani wa kibiashara na kuongeza mapato.

Waziri Kairuki aliyasema hayo hivi karibuni alipofanya ziara yake ya kikazi katika Shirika hilo iliyolenga kufanya mapitio ya utendaji wa shirika na kujadili mikakati ya kulifanya liendane na mahitaji ya sasa ya Uchumi wa kidijitali.

Akiambatana na Naibu Waziri, Mhe. Dkt. Switbert Mkama (Mb), Naibu Katibu Mkuu, Bw. Nicolaus Mkapa, pamoja na Menejimenti ya Wizara, Mhe. Kairuki alipokea taarifa ya utendaji iliyowasilishwa na Mkurugenzi Mkuu, CPA Moremi Marwa.

Katika ziara hiyo, Waziri alitembelea miundombinu ya kimkakati ambayo ni pamoja na Network Operation Center (NOC) na National Internet Data Centre (NIDC) miundombinu inayosimamiwa na kuendeshwa na TTCL kwa maslahi mapana ya Taifa. 

Akizungumza baada ya kukamilika kwa ziara, Mhe. Kairuki aliwapongeza Watumishi wa TTCL kwa hatua kubwa za maendeleo zilizofikiwa, huku akisisitiza umuhimu wa kuongeza kasi ya uboreshaji wa huduma ili kuhakikisha wananchi mijini na vijijini wanapata mawasiliano ya uhakika. 

Katika hatua nyingine Waziri Kairuki alilitaka shirika hilo kuona umuhimu wa kuongeza watumishi, kuwajengea uwezo, kuboresha miundombinu, na kuwekeza katika huduma za data zinazochochea uchumi wa kidijitali.

Kwa upande wake, Naibu Waziri, Mhe. Dkt. Switbert Mkama (Mb), aliitaka TTCL kuimarisha ubora wa huduma zinazotolewa kupitia minara ili kupunguza changamoto za mtandao hafifu, hususan vijijini na kuhimiza utafutaji wa masoko mapya ya Mkongo wa Taifa pamoja na kuendeleza ubunifu utakaoisaidia TTCL kubaki katika ushindani wa soko.

Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, CPA Moremi Marwa, alimshukuru Mhe. Waziri kwa ziara hiyo na maelekezo aliyoyatoa, akiahidi kuwa shirika litaendelea kuongeza ubunifu, kuboresha huduma kwa wananchi na kusimamia kikamilifu miundombinu ya taifa. 

Moremi alibainisha kuwa TTCL ina dhamira ya kuwa Taasisi ya kisasa inayokwenda sambamba na mahitaji ya maendeleo ya kidijitali kwa manufaa ya watanzania.