info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

WATUMISHI WAHIMIZWA KUIMARISHA UWAJIBIKAJI KWA HUDUMA ENDELEVU KWA WANANCHI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Jakaya Kikwete (Mb), amezindua rasmi Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2026 yanayofanyika katika Viwanja vya Chinangali Park, jijini Dodoma, huku akiwataka watumishi wa umma nchini kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uwajibikaji na kujituma katika kutoa huduma bora na endelevu kwa wananchi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mhe. Kikwete alisisitiza umuhimu wa watumishi wa umma kuzingatia maadili ya utumishi na kuwahudumia wananchi kwa ufanisi sambamba na kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu isemayo “Kuchochea Uwajibikaji kwa Huduma Endelevu.”

Maadhimisho hayo yanawakutanisha taasisi mbalimbali za umma na binafsi kwa lengo la kuonesha huduma wanazotoa, kubadilishana uzoefu na kuimarisha uhusiano kati ya taasisi na wananchi.

Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) ni miongoni mwa taasisi zinazoshiriki kikamilifu katika maonesho hayo, ambapo linaendelea kuonesha mchango wake katika kuimarisha mawasiliano ya uhakika na kuendeleza ajenda ya Tanzania ya kidijitali kupitia huduma na suluhisho mbalimbali za mawasiliano.

Kupitia banda lake, TTCL inatoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma zake mbalimbali, ikiwemo Faiba Mlangoni Kwako (FTTH), huduma za simu ya mkononi, T-PESA, huduma za intaneti kwa taasisi na mashirika, pamoja na huduma za kuhifadhi data kimtandao kupitia Kituo cha Kuhufadhi Data kimtandao (NIDC). 

Aidha, Shirika linaendelea kutoa huduma ya intaneti ya Wi-Fi katika mabanda mbalimbali ya taasisi zinazoshiriki maonesho hayo, hatua inayowezesha mawasiliano na upatikanaji wa taarifa kwa urahisi zaidi wakati wote wa maadhimisho.

Ushiriki wa TTCL katika Wiki ya Utumishi wa Umma unaonesha dhamira ya Shirika ya kuendelea kusaidia utoaji wa huduma bora kwa wananchi kupitia miundombinu na teknolojia za kisasa za mawasiliano, sambamba na kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.