WANAWAKE WA TTCL WATOA MSAADA JKCI MAADHIMISHO YA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI
Katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, Wanawake wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) wametoa msaada wa vifaa mbalimbali katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya kuonesha mshikamano na kuwafariji watoto pamoja na wazazi wanaopatiwa matibabu katika taasisi hiyo.
Msaada huo umejumuisha vifaa muhimu vitakavyosaidia watoto na wazazi wao wakati wakiendelea na matibabu, ikiwemo taulo za kike, pampas pamoja na maziwa kwa ajili ya watoto wachanga.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo kwa uongozi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Afisa Uhusiano Mwandamizi wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Adeline Berchimance alisema wanawake wa TTCL wamefika katika taasisi hiyo kuonesha mshikamano na kutoa faraja kwa Watoto wagonjwa na wazazi wao.
“Kwa niaba ya Wanawake wote wa TTCL tumefika hapa kuonesha mshikamano wetu. Tunatambua kuwa safari ya matibabu si rahisi, hivyo tumekuja hapa si kutoa msaada tu bali pia kutoa neno la faraja kwa wenzetu waliopo katika kituo hiki,” alisema.
Aidha, aliwapongeza wataalamu na wahudumu wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kwa kuendelea kujitoa kwa moyo mkubwa katika kuhakikisha watoto wanaoletwa katika taasisi ya JKCI wanapata huduma bora na kuendelea kuwa salama.
Aliongeza kuwa ingawa msaada huo unaweza usitosheleze mahitaji yote yaliyopo, ni ishara ya upendo, mshikamano na kujali kutoka kwa wanawake wa TTCL pamoja na familia nzima ya shirika la Mawasiliano Tanzania kwa jamii tunayoihudumia.“TTCL tunaamini kuwa mafanikio ya taasisi hayawezi kutenganishwa na ustawi wa jamii. Ndiyo maana mbali na kutoa huduma za mawasiliano kote nchini, shirika limeendelea kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii zinazogusa maisha ya Watanzania,”
Kwa miaka mbalimbali TTCL imekuwa likifanya shughuli za kijamii mara kwa mara, ikiwemo kutoa msaada katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, kuchangia damu pamoja na kuwasaidia wanawake wajasiriamali wa Soko la Mabibo kwa kuwapatia vifaa na vitendea kazi ili kuboresha mazingira ya shughuli zao.
Kwa upande wake, Dkt. Naizihijwa Majani kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete aliwashukuru wanawake wa TTCL kwa kuichagua taasisi hiyo na kutambua umuhimu wa kutoa msaada kwa wazazi na watoto.
“Napenda kuwashukuru wanawake wa Shirika la Mawasiliano Tanzania - TTCL pamoja na uongozi wao kwa kutambua umuhimu wa kuja kutoa misaada hii katika taasisi hii. Baadhi ya wazazi na watoto wamekuwa na upungufu wa vifaa kutokana na kukaa muda mrefu wakipatiwa matibabu, hivyo msaada huu utawagusa moja kwa moja walengwa na tunapenda kuwapongeza tena na tena kwa kufanya jambo hili kubwa,” alisema.
Naye Bi. Becky Kiabala Lukelo akizungumza kwa niaba ya wanufaika wa msaada huo ameishukuru TTCL kupitia Watumishi wake Wanawake kwa kujali na kutambua mahitaji ya watoto wanaopatiwa matibabu katika taasisi hiyo, akisema kuwa msaada huo utakuwa na manufaa makubwa kwao wakati wa matibabu.
Katika hatua nyingine, wanawake wa TTCL walipata pia fursa ya kuchangia damu na kupima afya zao kupitia madaktari bingwa wa moyo wanawake kutoka JKCI, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha umuhimu wa uchunguzi wa afya ya moyo kwa wanawake na kuokoa maisha kwakuchangia damu.