WANAWAKE - TTCL WAPATIWA SEMINA YA AFYA YA AKILI KUELEKEA MAADHIMISHO YA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI
Katika kuadhimisha na kuelekea kilele cha Siku ya Wanawake Duniani mwaka huu 2026, Wanawake wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) wamepatiwa semina maalum ya Afya ya Akili na Magonjwa Sugu Yasiyoambukiza lengo likiwa ni kuimarisha ustawi wa kisaikolojia, kuongeza uelewa kuhusu changamoto za afya ya akili, magonjwa sugu na kuhamasisha mazingira bora ya kazi yanayojali ustawi wao kama Watumishi wa Umma.
Semina hiyo imefanyika Machi 4, mwaka huu Makao Makuu ya Shirika hilo huku Wanawake nje ya Mkoa wa Dar es Salaam wakishiriki kwa njia ya mtandao ikitoa fursa kwa ushiriki mpana na mjadala shirikishi.
Akitoa mada katika semina hiyo, Dkt. Kweka Garvin, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Figo na Elimu ya Afya ya Akili na Msongo wa Mawazo kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, alieleza kwa kuna umuhimu wa kulinda afya ya akili kama nyenzo muhimu ya kuongeza tija kazini na kuboresha maisha binafsi.
Aliwapa mbinu za kukabiliana na msongo wa mawazo, kujenga ustahimilivu (resilience), pamoja na kudumisha uwiano kati ya majukumu ya kikazi na maisha ya kifamilia.
Katika hatua nyingine Dkt. Kweka Aidha, aliwahimiza Wanawake hao kujenga utamaduni wa kuzungumza wazi kuhusu changamoto za kihisia na kutafuta msaada wa kitaalamu pale inapohitajika.
Akizungumza kwa niaba ya Kamati ya Wanawake TTCL, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Bi. Mercy Amani, aliishukuru Menejimenti ya Shirika kwa kuwezesha semina hiyo na kuonesha dhamira ya dhati katika kuwekeza kwenye ustawi wa wanawake ndani ya shirika hilo. Pia aliwapongeza wanawake wa TTCL nchi nzima kwa kujitokeza kwa wingi na kushiriki kikamilifu katika mafunzo hayo.
Bi. Amani aliwasisitiza washiriki kutumia maarifa na mbinu walizojifunza si tu katika kulinda afya ya akili, bali pia katika kujikinga na magonjwa sugu yasiyoambukizwa yanayoweza kuathiri utendaji wao kazi na kuathiri mfumo mzima wa maisha yao.
Alieleza kuwa mwanamke mwenye afya bora ya akili na mwili ni nguzo muhimu ya Shirika familia na jamii kwa ujumla na kwamba ustawi wao utaongeza tija, uwajibikaji na ufanisi ndani ya Shirika.
Semina hiyo ni sehemu ya maandalizi ya TTCL katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, na inaakisi dhamira ya Shirika katika kuendeleza rasilimali watu kwa mtazamo wa ustawi jumuishi ili kuhakikisha wanawake wanakuwa na mazingira wezeshi ya kufikia malengo yao binafsi na ya shirika kwa ufanisi zaidi.