info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

WANAWAKE TTCL WAADHIMISHA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI

Katika kuunga mkono ajenda ya kimkakati ya Serikali ya kuimarisha usawa wa kijinsia na kuongeza ushiriki wa wanawake katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii, Wanawake Wafanyakazi wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kutoka Mikoa mbalimbali nchini wameshiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani 2026. 

Maadhimisho hayo yamefanyika ngazi ya Mkoa  huku wanawake wa TTCL kutoka Mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Mbeya, Kilimanjaro na mingine wakishiriki maadhimisho hayo kulingana na kila mkoa ulivyopanga.

Kwa upande wa Mkoa wa Dar es Salaam, wanawake wa TTCL waliungana na wanawake wengine wa Mkoa huo katika maadhimisho yaliyofanyika katika Viwanja vya Barafu vilivyopo Mburahati jijini Dar es Salaam. 

Maadhimisho ya mwaka huu yameongozwa na kaulimbiu isemayo “Haki na Usawa kwa Wanawake na Wasichana: Msingi Jumuishi Kufikia Dira ya Maendeleo 2050,” inayolenga kuhimiza usawa wa kijinsia, uwezeshaji wa wanawake pamoja na kutambua mchango wao katika maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.

Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Chalamila, ambaye alikuwa mgeni rasmi, aliwapongeza wanawake wa Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na wanawake wote nchini kwa mchango wao mkubwa katika maendeleo ya Taifa. 

Alisema wanawake wameendelea kuwa nguzo muhimu katika utekelezaji wa majukumu ya kikazi na katika kuimarisha ustawi wa jamii na familia.

“Wanawake wamekuwa mstari wa mbele sana katika ufanyaji kazi na ulinzi wa jamii kwa ujumla, ikiwa ni pamoja na kulinda familia na kufanya kazi kwa bidii hali inayopelekea ukuaji wa kasi wa taifa,” alisema Chalamila.

Akizungumza kwa niaba ya wanawake wa TTCL, Mwenyekiti wa Kamati ya Wanawake Wafanyakazi wa TTCL, Bi. Mercy Ngoda, alisema wanawake wa shirika hilo wataendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuleta maendeleo ya taifa kupitia utoaji wa huduma bora za mawasiliano pamoja na kushiriki katika shughuli za kijamii.

Siku ya Wanawake Duniani huadhimishwa kila mwaka tarehe 8 Machi, ikiwa ni jukwaa muhimu la kutambua mchango wa wanawake katika maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa, pamoja na kuhimiza juhudi za pamoja za kufanikisha usawa wa kijinsia duniani.