info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

WAJUMBE WA BODI YA TTCL WAKAGUA UTEKELEZAJI WA KAMPENI YA “FAIBA MLANGONI KWAKO” KIMARA

Wajumbe wa Bodi ya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) wamefanya ziara ya ukaguzi katika eneo la Kimara, jijini Dar es Salaam, ili kujionea maendeleo ya utekelezaji wa Kampeni ya “Faiba Mlangoni Kwako”. 

Ziara hiyo imelenga kuhakikisha utekelezaji wa kampeni hiyo inakwenda sambamba na malengo ya kuongeza upatikanaji wa huduma za mawasiliano ya kasi kwa wananchi na wafanyabiashara.

Katika ziara hiyo, wajumbe wa Bodi wamelitaka TTCL kuhakikisha inaunganisha wateja moja kwa moja katika makazi na biashara zao, ili kuongeza ufanisi na manufaa ya mradi na kuongeza kuwa utekelezaji wa haraka utachangia kuongeza wigo wa huduma za mawasiliano na kuchochea ukuaji wa uchumi wa kidijitali nchini.

Kampeni ya “Faiba Mlangoni Kwako” katika eneo la Kimara inahusisha maeneo ya Kimara Stopover, Kimara Baruti, Kimara Temboni na Kimara Kibanda cha Mkaa ambapo kupitia kampeni hii, wananchi wa maeneo hayo watapata huduma za mawasiliano ya kisasa zenye kasi na uhakika, zitakazowawezesha kupata taarifa kwa urahisi na kuboresha mifumo ya biashara na maisha ya kila siku.

Huduma zitakazotolewa kupitia kampeni hii zinatarajiwa kuchochea maendeleo ya kidijitali, kuongeza tija katika shughuli za biashara, kuboresha utoaji wa huduma za kijamii na kuinua ubora wa makazi (Smart home) ambapo TTCL inatekeleza mradi huu kwakuwajengea miundo mbinu bure ili kuwapa wananchi fursa ya kushiriki kikamilifu katika fursa za uchumi wa kidijitali.

TTCL imejidhatiti kuendelea kusogeza huduma zake karibu zaidi na wananchi ili  kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora, za haraka na zenye usalama wa taarifa na Faiba mlangoni ni hatua muhimu katika kuifikisha Tanzania kwenye uchumi wa kidijitali.

Bodi ya Wakurugenzi ya TTCL imeonesha dhamira yake ya kuendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi mikubwa ya mawasiliano ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati, inakidhi viwango vya ubora na inaleta manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi, sambamba na mkakati wa kitaifa wa kuendeleza uchumi wa kidigitali.