WAFANYAKAZI 14 WA TTCL NA KINAPA WAPEWA TUZO
Wafanyakazi 14 wa TTCL na KINAPA watunukiwa tuzo maalum kwa kufanikisha ujenzi wa mawasiliano ya Intaneti katika kilele cha Mlima Kilimanjaro. Tuzo zimetolewa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia, Mhe. Nape Moses Nnauye katika hafla iliyofanyika Marangu Gate Mkoani Kilimanjaro, Julai 22 mwaka huu na kuhudhuriwa na Viongozi kutoka taasisi na mashirika mbalimbali Wafanyakazi hao wamefanikisha Ujenzi wa kilometa 42.5 za Mkongo wa Mawasiliano ya Intaneti katika Mlima Kilimanjaro kuanzia kituo cha Marangu Gate, Mandara (2720m), Horombo (3720m), Kibo (4720m), Gilman’s (5685m), Stella (5756m), hadi Kilele cha Mlima Kilimanjaro Uhuru Peak (5895m). Mhe. Nape amesema kuwa kukamilika kwa mradi huu ni hatua kubwa katika Taifa letu na duniani kwa ujumla kushuhudia Mlima Mrefu Afrika kuwa na mawasiliano ya Intaneti, utafungua fursa za kukuza utalii na kutengeneza mazingira rafiki kwa watalii kupata huduma za mawasiliano wawapo kwenye shughuli za utalii. “Nawapongeza Wafanyakazi wa TTCL kumi na moja (11) na Wafanyakazi wa KINAPA wa Tatu(3) na wengine walioshiriki namna moja au nyingine kwa kazi kubwa waliyoifanya ya ujenzi wa mawasiliano, natambua ugumu na hali ya hewa ya Mlima Kilimanjaro, lakini jitihada zenu zimefanikisha ujenzi huu ambao hivi sasa huduma za mawasiliano zinapatikana katika Mlima Kilimanjaro” amesema Mhe. Nape Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL, Bi Zuhura Sinare Muro pia amewapongeza Wafanyakazi na wadau wote walioshiriki katika kufanikisha mradi huu, tunatambua changamoto ya hali ya hewa iliyopo katika Mlima huu lakini kwa umoja na uzalendo wenu mkakamilisha mradi huu. “Tunaimani kuwa TTCL itakuwa na mchango mkubwa katika kuunga mkono juhudi za serikali za kutangaza vivutio vya utalii na kuimarisha mawasiliano kwenye maeneo yote ya hifadhi za utalii nchini” amesema Bi. Zuhura Muro Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Mhandisi Peter Ulanga amesema kuwa Shirika linatambua mchango wa wafanyazi katika kukamilisha mradi huu mawasiliano hadi katika kilele cha Kilimanjaro “Hii inaonesha jinsi tulivyopiga hatua kama Taifa yakuwa na wataalam wa kuweza kufanya kazi hizi bila kuhitaji msaada wa wataalamu kutoka nje ya nchi. Kwa mara nyingine naomba ninawashukuru na kuwapongeza kwa weledi waliouonesha katika kukamilisha mradi huu kwa wakati” amesema Mhandisi Peter Ulanga