WADAU WA SEKTA YA MAWASILIANO NA TEHAMA WATAKIWA KUIUNGANISHA AFRIKA
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry Slaa (Mb) amewataka Wadau wa sekta ya TEHAMA na Mawasiliano kuunganisha Afrika kwenye miundombinu ya mawasiliano ili kuchochea ukuaji wa ujenzi wa uchumi wa kidijitali utakaosaidia katika kuleta maendeleo kwa wananchi barani humo.
Waziri Silaa ametoa wito huo wakati akifungua Mkutano wa Kimataifa wa Mawasiliano na TEHAMA (Connect to Connect Summit 2024) Septemba 18, 2024 katika hoteli ya Gran Malia jijini Arusha.
Amewataka kuendelea kuimarisha ushirikiano uliopo kwa wadau wa sekta hiyo ya mawasiliano ili kufanikisha utekelezaji wa mikakati ya kuunganisha Afrika na kujenga uchumi wa kidijitali kwa nchi za bara hilo.
Akiwahitubia Wadau wa mkutano huo Mhe. Silaa amesema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuwekeza kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano- NICTBB ili kufanikisha ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano endelevu yenye kuleta tija kwa wananchi katika kupata huduma za intanet zenye ubora, bei nafuu na za kuaminika.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ufundi wa shirika la Mawasiliano Tanzania, Mhandisi Cecil Francis amesema katika kuhakikisha Afrika inaungwa kwenye miundombinu ya mawasiliano tayari Shirika hilo limefanikiwa kuunga nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki- EAC na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika- SADC kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ili kuwezesha nchi wanachama kukuza matumizi ya TEHAMA lengo likiwa ni kurahisisha shughuli za maendeleo.
Mhandisi Cecil ambaye alimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TTCL CPA Moremi Marwa amewaambia washiriki wa mkutano huo kuwa hivi sasa shirika hilo linaendelea na juhudi za kuunganisha nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo- DRC kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kupitia ziwa Tanganyika mkoani Kigoma hadi katika jimbo la Kalemie DRC na kwamba kukamilika kwake kutakuwa kumekamilisha Mpango Mkakati wa serikali wa kuziunganisha nchi zote zinazopakana na tanzania katika Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.
Amesema kukamilika kwa kazi hii kutasaidia kukuza ushiriakiano wa Kikanda katika kuchochea ukuaji wa maendeleo.
Aidha Mhandisi Cecil amesema kuwa Shirika limeendelea na juhudi za kuboresha miundombinu ya mawasiliano sambamba na kuunganisha zaidi ya Wilaya 100 kati ya 139 katika Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ili kuchochea kasi ya ujenzi wa Tanzania ya Kidigitali na kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Mkutano huu wa Kimataifa wa C2C hufanyika kila mwaka ukiwa na lengo la kuwa kuwakutanisha Viongozi, Wataalam, Kampuni na Wadau wengine wa TEHAMA kutoka nchi mbalimbali duniani ambapo wadau hao hutumia fursa hiyo kujadili, kupanga na kubadilishana uzoefu kuhusu mabadiliko na ukuaji wa Teknolojia ya mawasiliano duniani.