VIONGOZI WA BODI YA T-PESA WATEMBELEA BANDA LA TTCL SABASABA 2026
Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL-PESA Bw. Richard Mayongela akiongozana na Wajumbe wengine wametembelea Banda la Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba 2026), ambapo walijionea huduma mbalimbali za kidijitali na suluhisho za kifedha zinazotolewa kupitia T-PESA kwa wananchi, taasisi na wafanyabiashara.
Katika ziara hiyo, viongozi hao walipokea maelezo kuhusu mchango wa T-PESA katika kurahisisha huduma za kifedha kwa kutumia teknolojia ya kidijitali, ikiwa ni pamoja na kutuma na kupokea fedha kwenye mitandao yote ya simu, kufanya malipo ya biashara kwa urahisi, pamoja na huduma za Cash Disbursement zinazowawezesha taasisi, makampuni, vikundi vya wakulima na vyama vya ushirika kufanya malipo kwa mkupuo kwa ufanisi na usalama.
Aidha, walijionea namna huduma za T-PESA zinavyoendelea kuwa kichocheo cha ukuaji wa uchumi wa kidijitali kwa kuwezesha wananchi na wafanyabiashara kufanya miamala kwa haraka, salama na kwa urahisi, bila kujali mahali walipo.
Viongozi wa Bodi walipongeza juhudi zinazoendelea kufanywa na TTCL na T-PESA katika kubuni na kuboresha huduma za kidijitali zinazokidhi mahitaji ya soko na kuimarisha ujumuishi wa kifedha nchini.
TTCL inaendelea kutumia Maonesho ya Sabasaba 2026 kama jukwaa la kuonesha suluhisho bunifu za mawasiliano na huduma za kifedha zinazochangia maendeleo ya biashara, uwekezaji na ukuaji wa uchumi wa kidijitali nchini.