info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

VIJANA WAHUSISHWE KATIKA MIJADALA YA UTAWALA WA MTANDAO AFRIKA-MHANDISI MAHUNDI

Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Meryprisca Mahundi (Mb), Mei 29 mwaka huu alfungua rasmi vikao vya awali vya majadiliano vya Wabunge na Vijana kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika, wanaoshiriki Mkutano Mkuu wa Jukwaa la Usimamizi wa Mtandao Barani Afrika (African Internet Governance Forum - AfIGF), unaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC).

Akizungumza mbele ya wabunge zaidi ya 40 kutoka Mataifa mbalimbali, Mhandisi Mahundi alieleza jinsi matumizi ya data na intaneti yanavyozidi kuwa na umuhimu mkubwa kwa taifa, pamoja na juhudi mbalimbali zinazofanyika kuhakikisha matumizi sahihi ya teknolojia hiyo miongoni mwa watumiaji nchini. 

Mhandisi Mahundi amesisitiza umuhimu wa kuwahusisha na kuwashirikisha vijana katika mjadala wa utawala wa mtandao, kuhusu sera, usalama, na usimamizi wa mtandao barani Afrika, akisema kuwa vijana ni nguvu kazi muhimu na bunifu katika mabadiliko ya kidijitali.

Mkutano huo wa awali unalenga kuandaa mazingira rafiki ya ushirikiano kati ya watunga sera (wakiwemo wabunge) na kizazi kipya cha watumiaji na wabunifu wa teknolojia (Vijana) ambapo kumekuwepo na majadiliano yanahusisha mada mbalimbali kama vile sera za faragha mtandaoni, usalama wa taarifa, fursa za kijamii na kiuchumi kupitia teknolojia, pamoja na changamoto za upatikanaji wa intaneti vijijini.

Katika hatua nyingine, Mhandisi Mahundi amewahimiza vijana kutumia data kwa matumizi chanya, hususan katika kuonyesha uwezo wao katika kubuni kazi mbalimbali kwakutumia TEHAMA huku akiwahakikishia kuwa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imekuwa mstari wa mbele katika kuwawezesha vijana kuonesha bunifu zao kiteknolojia.

“Tumewashirikisha moja kwa moja vijana. Kama mnavyojua, katika wizara yetu tumekuwa tukiwawezesha sana vijana na kuibua vipaji pamoja na ubunifu wao” Amesema Mhandisi Mahundi. 

Amesema vijana wanaposhirikishwa katika mijadala mbalimbali inakuwa ni chachu kwao kwani wao ndiyo watumiaji wakubwa wa intaneti, hivyo, wanapata uelewa kuwa wanapaswa kuzingatia matumizi chanya ya mitandao kwa mustakabali bora wa Taifa.

AfIGF ni jukwaa la wadau wa intaneti ambapo serikali, Mashirika, Taasisi, sekta ya binafsi na jumuiya za kiufundi na kibunifu hujadili vipaumbele vya kidijitali vya Afrika. Jukwaa hili liliadaliwa na Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa lengo likiwa ni kuleta sauti za bara hilo katika ngazi ya kimataifa na kuhakikisha manufaa ya mtandao thabiti yanamfikia kila mtu.