TUMIENI HUDUMA ZINAZOZALISHWA NCHINI KWA MAENDELEO YA TAIFA-MAYONGELA
Wito umetolewa kwa Wananchi kutumia huduma zinazozalishwa hapa nchini ili kuchochea maendeleo na kukuza uchumi wa Taifa.
Wito huo ameutoa na Mwenyekiti wa Bodi ya T-PESA ambayo ni Kampuni Tanzu ya Shirika la Mawasiliano Tanzania – TTCL, Bw. Richard Mayongela alipotembelea Banda la TTCL wakati wa Maonesho ya Nanenane yaliyofanyika katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Bw. Mayongela alisema kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, umepelekea kuwepo na huduma bora zinazotolewa na shirika hilo kwa Wananchi.
Aliwataka Watanzania na wadau mbalimbali kutumia huduma za TTCL ambapo kwa sasa shirika hilo linatoa huduma ya intanet majumbani na kwamba kwakutumia huduma hiyo faida itakayopatikana itarejeshwa kwa Wananchi wenyewe kupitia huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na elimu, afya na miundombinu.
Alisema kwa uwekezaji mkubwa uliofanyika sasa ndani ya shirika hilo huduma ya internet inaunganishwa kwenye Majengo ya Serikali kuwezesha shughuli mbalimba za serikali katika kuwahudumia Wananchi kufanyika kwa haraka, ubora na kuongeza ufanisi katika utoaji huduma.
Akizungumzia huduma ya Lipa kwa Mkupuo kupitia T-PESA Bw. Mayongela alisema shirika limekuja na huduma hiyo kwa madhumuni ya kurahisisha malipo kwa Wakulima, Wafanyabiashara na wadau mbalimbali ambao wanahitaji kuwalipa watu wengi.
"Shirika limekuja na huduma hii kwa madhumuni ya kurahisisha malipo badala ya mtu kubeba pesa na kumlipa mtu mmoja mmoja sasa unaweza kulipa wote kwa mkupuo kupitia mfumo maalum",alisema Mayongela