info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

TTCL YAZINDUA KIJITONYAMA FTTX EXPERIENCE CENTER

Mwenyekiti wa Bodi wa Shirika la Mawasiliano Tanzania -TTCL amezindua rasmi kituo cha kisasa cha maonesho kinachojulikana kama KIJITONYAMA FTTX Experience Center chenye lengo la kuonesha na kuelimisha umma kuhusu teknolojia ya mawasiliano ya kisasa.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika hilo David Carol Nchimbi amepongeza juhudi za Menejimenti chini ya uongozi wa Mkurugenzi Mkuu kwa kubuni na kutekeleza wazo la kuanzisha kituo hicho, ambacho kinalenga kuonesha na kuelimisha umma kuhusu teknolojia ya mawasiliano ya kisasa majumbani, ofisini pamoja na sehemu mbalimbali.

“TTCL tumejipanga kuhakikisha Watanzania wanaunganishwa kikamilifu na dunia kupitia huduma bora za mawasiliano. Kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, tunahudumia wadau mbalimbali nchini, na sasa kupitia teknolojia ya FTTH, tunapeleka huduma za intaneti moja kwa moja majumbani na ofisini,” amesema Nchimbi.

Aliongeza kuwa katika dunia ya sasa, matumizi ya intaneti hayaishii kwenye simu pekee, bali yanapanuka hadi majumbani kupitia mifumo ya Smart Home, inayowezesha watumiaji kudhibiti vifaa mbalimbali kama taa, mashine za kufulia, mapazia, mifumo ya ulinzi pamoja na burudani za kidijitali kwa kutumia mtandao.

Katika hatua nyingine Nchimbi, ametoa shukrani kwa washirika wa kimkakati wa uanzishwaji wa TTCL FTTX Experience Center, kampuni za Huawei na Hisense, kwa ushirikiano wao mkubwa uliofanikisha kuanzishwa kwa kituo hicho.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania - TTCL Bw. Moremi Marwa ameeleza kuwa uzinduzi wa kituo hicho ni sehemu ya mkakati wa shirika wa kuboresha huduma kwa wateja na kuongeza mapato hali itakayopelekea shirika kuweza kujiesha kwa faida.

“Kituo hiki kitatoa fursa kwa wateja kupata uzoefu wa moja kwa moja wa huduma zetu za Intaneti za Majumbani pamoja na Ofisini. Hii ni njia mojawapo ya kuvutia masoko kwa kuonesha kwa vitendo ubora wa huduma tunazotoa,” alisema Marwa.

Alisisitiza kuwa TTCL inaendelea kutekeleza maelekezo ya Serikali ya kuhakikisha shirika linaendeshwa kwa ufanisi na faida, akibainisha kuwa baada ya kupata faida mwaka jana, matarajio ni kuendeleza mwenendo huo chanya mwaka huu wa kuhakikisha shirika linaendelea kuendeshwa kwa kuingiza faida na sio kupata hasara kama ilivyokuwa kwa miaka kadhaa nyuma.

Uzinduzi wa TTCL FTTX Experience Center unatarajiwa kuwa kichocheo muhimu katika kuharakisha upatikanaji wa huduma za mawasiliano ya kisasa nchini, pamoja na kuhamasisha matumizi ya teknolojia za kidijitali katika maisha ya kila siku ya Watanzania.