TTCL YAWEZESHA MAWASILIANO YA KIDIJITALI KATIKA KIKAO KAZI CHA WENYEVITI WA BODI NA WAKUU WA TAASISI
Na Adeline Berchimance
Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) linaendelea kuonesha nafasi yake muhimu katika kuwezesha shughuli za Serikali kidijitali kwa kutoa huduma ya intaneti yenye uhakika katika Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Wakuu wa Taasisi (Chairpersons and CEOs Forum) kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Kikao hicho kinachofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC) kimefunguliwa rasmi leo na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndenjembi kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Katika kufanikisha kikao hicho, TTCL imetoa huduma ya intaneti inayowawezesha washiriki kupata na kubadilishana taarifa kwa wakati, kufanya mawasiliano ya kidijitali, pamoja na kushiriki mijadala na shughuli mbalimbali zinazohitaji huduma za mtandao.
Upatikanaji wa huduma hiyo unaongeza ufanisi katika utekelezaji wa shughuli za kikao na kuwezesha washiriki kutumia mifumo na majukwaa mbalimbali ya kidijitali kwa urahisi na uhakika.
Ushiriki wa TTCL katika kikao hiki unaakisi dhamira ya Shirika ya kuendelea kuwa mhimili muhimu wa mawasiliano nchini kwa kuiwezesha Serikali, Taasisi na Mashirika ya Umma kupata miundombinu na huduma za mawasiliano zinazochochea ufanisi katika utendaji, ushirikiano na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Aidha, kupitia uwekezaji na utoaji wa huduma za mawasiliano ya kisasa, TTCL inaendelea kuchangia utekelezaji wa ajenda ya Mageuzi ya Kidijitali Tanzania kwa kuhakikisha teknolojia na huduma za mawasiliano zinatumika kama nyenzo muhimu ya kuongeza tija, uwajibikaji na ufanisi katika shughuli za Serikali.
Kikao hicho cha siku tatu kinawakutanisha Wenyeviti wa Bodi, Wakuu wa Taasisi na viongozi mbalimbali kwa lengo la kujadili masuala ya kimkakati yanayohusu uongozi, uwajibikaji, utawala bora na uboreshaji wa utendaji wa Taasisi na Mashirika ya Umma nchini.
#TTCL #CEOsForum #AICCArusha #DigitalTanzania #MageuziYaKidijitali #Uongozi #Uwajibikaji