info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

TTCL YAWEKA MIKAKATI MADHUBUTI KUFANIKISHA DIRA YA MAENDELEO 2050

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Bw. Moremi Marwa, amewasilisha mafanikio ya shirika pamoja na mikakati yake ya kimkakati katika kufikia Dira ya Maendeleo 2050 wakati wa kikao kazi kilichoandaliwa na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na wadau wa sekta ya Mawasiliano na TEHAMA nchini.

Kikao kazi hicho kilichofanyika Februari 26 mwaka huu 2026 jijini Dodoma, kililenga kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi, kujadili fursa na changamoto za maendeleo ya TEHAMA, pamoja na kuweka mikakati ya pamoja ya kuharakisha mageuzi ya kidijitali kwa ustawi wa Taifa.

Miongoni mwa Taasisi na Mashirika yaliyo chini ya Wizara yaliyoshiriki kikao hicho ni Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Shirika la Posta Tanzania (TPC), ICT Commission pamoja na TTCL. Taasisi hizo zilieleza mchango wao katika kuimarisha upatikanaji wa huduma za mawasiliano na TEHAMA mijini na vijijini.

Aidha, kwa upande wa sekta binafsi kampuni mbalimbali za mawasiliano na teknolojia ikiwemo Vodacom Tanzania, Airtel Tanzania, Halotel Tanzania, Yas, Sahara Veture, Helois Tower, Towerco Africa, Huawei, RADDY Fiber pamoja na wadau wengine. Ushiriki wao ulilenga kujadili uwekezaji, ubunifu na namna ya kuimarisha ushindani wenye tija katika soko la mawasiliano.

Akitoa wasilisho katika kikao hicho, Bw. Marwa alieleza kuwa TTCL imeendelea kuimarisha miundombinu ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, kupanua huduma za intaneti ya kasi, pamoja na kuanzisha suluhisho bunifu zitakazosaidia sekta mbalimbali za uchumi kuingia kikamilifu katika uchumi wa kidijitali. 

Alisisitiza kuwa mafanikio hayo ni sehemu ya safari ya kuhakikisha Tanzania inafikia malengo ya Dira ya Maendeleo 2050.

Akihitimisha wasilisho lake, Bw. Marwa aliwaalika watoa huduma za mawasiliano na wadau wengine kutumia huduma mpya ya “Fiber to the Site” inayotolewa kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, ambao umepita karibu na minara ya mawasiliano nchini na kuongeza kuwa huduma hiyo itasaidia kupunguza gharama za uendeshaji, kuongeza ubora wa huduma, na kuimarisha upatikanaji wa mawasiliano ya uhakika kwa wananchi na Taasisi mbalimbali.