info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

TTCL YAWASHUKURU WATEJA NA WADAU, YAWAKARIBISHA KUENDELEA KUTUMIA HUDUMA ZAKE

Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limewashukuru wananchi, wateja na wadau mbalimbali kwa mwitikio mkubwa waliouonesha kwa kutembelea Banda Na. 26 la TTCL katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam, maarufu kama Sabasaba.

Maonesho hayo yalifanyika kuanzia tarehe 28 Juni hadi 13 Julai 2026 katika Viwanja vya Maonesho vya Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam.

Akizungumza mara baada ya kufungwa rasmi kwa maonesho hayo, Meneja wa Banda la TTCL, Bi. Janeth Maeda, amesema ushiriki mkubwa wa wananchi uliipa TTCL fursa ya kuonesha huduma, bidhaa na suluhisho mbalimbali za kidijitali zinazochangia maendeleo ya uchumi wa kidijitali nchini.

Amesema wananchi waliotembelea banda hilo walipata elimu na taarifa kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na TTCL, ikiwemo Faiba Mlangoni Kwako, Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB), Public Wi-Fi, Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Data (NIDC), huduma za Enterprise Business na Call Center Business.

Aidha, wageni walipata fursa ya kujionea kwa vitendo huduma na teknolojia mbalimbali kupitia Kituo cha Uzoefu wa Teknolojia ya FTTX, ambacho kinaonesha namna teknolojia za kisasa za mawasiliano zinavyoweza kutumika majumbani, katika biashara na kwenye taasisi mbalimbali.

Wananchi pia walipata elimu kuhusu huduma za kifedha kupitia T-PESA, sambamba na kunufaika na ofa maalumu za vifaa vya intaneti, vikiwemo Router, Dongle, Wingle na MiFi.

“Kwa namna ya pekee, tunawashukuru kwa dhati wananchi, wateja na wadau wote waliotembelea Banda la TTCL katika kipindi chote cha maonesho. Ushiriki wenu umeonesha imani kubwa mliyonayo kwa huduma zetu na umetupa hamasa ya kuendelea kubuni na kuboresha huduma zinazokidhi mahitaji ya Watanzania,” amesema Bi. Janeth.

Ameongeza kuwa TTCL itaendelea kuimarisha miundombinu ya mawasiliano na kutoa huduma zenye ubora, usalama na uhakika, ili kuwaunganisha Watanzania na kuchangia katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Bi. Janeth amewakaribisha wananchi, wateja na wadau kuendelea kutumia huduma mbalimbali za TTCL zinazopatikana katika ofisi za Shirika zilizopo kote nchini.

Pia, amewahimiza wananchi ambao hawakupata fursa ya kutembelea banda la TTCL wakati wa maonesho hayo kufika katika Kituo cha Uzoefu wa Teknolojia ya FTTX kilichopo Kijitonyama, Dar es Salaam, ili kujionea kwa karibu maendeleo na mapinduzi ya teknolojia ya mawasiliano yanayoendelea kutekelezwa na TTCL.