info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

TTCL YAWAPATIA MAFUNZO KWA WANAFUNZI WA CHUO CHA DIT

Wanafunzi wa Chuo cha DIT wameshauriwa kuweka bidii na maarifa katika masomo yao ili waweze kufikia malengo na kutimiza ndoto zao. 

Ushauri huo umetolewa na Fundi Sanifu Daraja la Pili wa Shirika la Mawasiliano Tanzania Bw. Isihaka Mwakatwira alipokuwa akitoa Mafunzo kwa Wanafunzi hao waliofika TTCL kujifunza masuala mbalimbali yanayohusu Teknolojia katika Sekta ya Mawasiliano nchini.

Isihaka aliwaambia wanafunzi hao kuwa wanapaswa kujifunza kwa bidii kwani TEHAMA ni fani inayobadilika kwa kasi, hivyo ni muhimu kujifunza mara kwa mara ili kukaa sambamba na maendeleo ya kiteknolojia.

Aliwataka kufanya mazoezi na kutekeleza Projekti wanazopewa na Walimu wao kwani maarifa ya TEHAMA yanahitaji mazoezi ya vitendo hivyo wanapaswa kuhakikisha wanafanya mazoezi ya programu, mifumo ya kompyuta, au hata uundaji wa tovuti ili kuimarisha ujuzi wako.

Aidha aliwaasa kutopuuza Vipindi vya mafunzo wanayopewa maana ni fursa muhimu ya kujenga msingi wa kazi ya baadaye na endapo wanahitaji eneo sahihi la kujifunza kwa vitendo masuala ya TEHAMA basi wasisite kulitumia Shirika la Mawasiliano Tanzania kutokana na ukweli kuwa ni kongwe lenye wataalam wengi hivyo watumie fursa ya uwepo wa shirika hilo kupata maarifa zaidi.

TTCL imejiwekea utaratibu wa kutoa Mafunzo kwa Wanafunzi wa Sekondari na vyuo ili kuwajengea uwezo Wanafunzi hao uelewa wa vitendo katika Teknolojia ya Mawasiliano ambapo Juni 19, 2024 jumla ya Wanafunzi 42 kutoka Chuo cha DIT walipatiwa mafunzo kwa vitendo.