TTCL YAWAKARIBISHA WANANCHI KUJIONEA NGUVU YA MAWASILIANO KATIKA MAONESHO YA NANENANE DODOMA
Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limeendelea kuwakaribisha wananchi, wafanyabiashara, taasisi za umma na binafsi kutembelea banda lake lililopo Government Pavilion 2, Viwanja vya John Malecela, Nzuguni jijini Dodoma, ili kujifunza na kujionea kwa karibu huduma na suluhisho mbalimbali za kisasa za mawasiliano na Teknolojia.
Katika banda hilo, wataalamu wa TTCL wanatoa elimu na maelezo kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na Shirika, zikiwemo huduma za intaneti ya kasi, huduma za simu, Cloud Computing, Data Centre pamoja na suluhisho mbalimbali za TEHAMA zinazolenga kukidhi mahitaji ya watu binafsi, wafanyabiashara na taasisi.
Ushiriki wa TTCL unalenga kuwapa wananchi fursa ya kufahamu namna teknolojia na huduma za kisasa za mawasiliano zinavyoweza kurahisisha shughuli za kila siku, kuongeza ufanisi katika biashara na taasisi, pamoja na kuchochea matumizi ya huduma za kidijitali nchini.
Wananchi wanaotembelea banda hilo pia wanapata nafasi ya kuzungumza moja kwa moja na wataalamu wa TTCL, kupata ushauri kulingana na mahitaji yao na kufahamu kwa kina namna wanavyoweza kuunganishwa na huduma mbalimbali za Shirika.
Aidha, TTCL inaendelea na ofa yake maalum ya modem na router kwa bei nafuu, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuwezesha wananchi wengi zaidi kupata huduma za intaneti na kunufaika na fursa zinazotokana na matumizi ya teknolojia ya kidijitali.
TTCL inaendelea kutumia fursa ya kukutana na wananchi ili kuimarisha uelewa kuhusu huduma zake, kusikiliza mahitaji ya wateja na kuonesha mchango wake katika kuendeleza mageuzi ya kidijitali na ukuaji wa uchumi wa Tanzania.