info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

TTCL YAUNGANISHA AFRIKA MASHARIKI KIDIJITALI KUPITIA TANZANIA–UGANDA CORRIDOR

Katika hatua ya kuimarisha mawasiliano ya kikanda na kukuza uchumi wa kidijitali, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa Tanzania, Mh. Jerry Silaa, ameongoza uzinduzi wa mradi wa kimkakati wa Tanzania–Uganda Corridor, hafla iliyoandaliwa na Kilimanjaro Telecoms.

Akizungumza katika tukio hilo, Mh. Silaa ameeleza dhamira ya Serikali kupitia TTCL kuendelea kuwekeza katika huduma za kasi ya juu za fiber optic, na kwamba Tanzania iko tayari kushirikiana na Uganda ili kukuza miundombinu ya TEHAMA itakayochochea maendeleo ya kanda.

"Tunataka kuona TTCL inakuwa daraja la kidijitali baina ya Tanzania na Uganda, na kwa kiwango kikubwa zaidi – Afrika Mashariki," alisema Mh. Silaa.

Aidha, Waziri alieleza kuwa TTCL ina mpango wa kuongeza uwezo wa huduma kupitia njia ya Kyaka – mpango utakaosaidia kupanua wigo wa mtandao, kuongeza kasi ya intaneti, na kuongeza upatikanaji wa huduma za kisasa za TEHAMA kwa nchi zote mbili.

Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na Waziri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wa Uganda, viongozi waandamizi kutoka mashirika ya mawasiliano ya umma na binafsi, pamoja na wadau wa sekta ya ICT kutoka pande zote mbili za mpaka.

Mradi huu wa “Tanzania–Uganda Corridor” unalenga: Kukuza ujumuishaji wa kidijitali wa kikanda, Kuwezesha biashara mtandao na mawasiliano ya haraka na Kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha TEHAMA Afrika Mashariki.