info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

TTCL YAUNGANA NA UONGOZI WA WILAYA YA ILALA KUFANYA USAFI WA MAZINGIRA JIJINI DAR-ES-SALAAM

Na Godfrey Andafiche

Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limeungana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala katika zoezi la usafi wa mazingira lililofanyika katika eneo la Posta, jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa dhamira ya Shirika ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), pamoja na kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha mazingira yanakuwa safi, salama na yenye kuvutia.

Zoezi hilo, lililoongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogolo, limewakutanisha viongozi na wafanyakazi wa TTCL pamoja na wadau wengine katika kuhamasisha ushiriki wa jamii kwenye shughuli za usafi na utunzaji wa mazingira.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mkurugenzi wa Ufundi wa TTCL, Mhandisi Cecil Francis, amepongeza uongozi wa Wilaya ya Ilala kwa kuendeleza juhudi za kuimarisha usafi wa mazingira, huku akisisitiza dhamira ya TTCL ya kuendelea kushirikiana na Serikali katika shughuli zinazochangia ustawi wa jamii.

Mhandisi Francis amesema ushiriki wa TTCL katika zoezi hilo ni sehemu ya kutekeleza wajibu wake kwa jamii, sambamba na jukumu lake la msingi la kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora na za uhakika za mawasiliano.

Aidha, ametumia fursa hiyo kuhamasisha wananchi kutumia huduma ya Faiba Mlangoni Kwako (FTTH) inayotolewa na TTCL, ambayo inawawezesha kupata intaneti ya kasi na ya uhakika kwa ajili ya kurahisisha mawasiliano, kuendesha biashara, kujifunza na kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogolo, ameipongeza TTCL kwa kujitokeza kushiriki katika zoezi hilo na kwa kuchangia vifaa vya usafi, akieleza kuwa ushirikiano wa taasisi na jamii ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha mazingira yanatunzwa kwa manufaa ya wananchi wote.

Mhe. Mpogolo amesema usafi wa mazingira ni agenda endelevu katika Wilaya ya Ilala, ambapo kila Jumamosi imetengwa kwa ajili ya kuhamasisha na kutekeleza shughuli za usafi katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.

Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Wilaya ameipongeza TTCL kwa kuzingatia utunzaji wa mazingira wakati wa utekelezaji wa miradi ya miundombinu ya mawasiliano, hususan shughuli za ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, kwa kuhakikisha maeneo yanayofanyiwa kazi yanarejeshwa katika hali ya usafi baada ya kukamilika kwa shughuli husika.

Amesisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano kati ya TTCL na uongozi wa Wilaya ya Ilala katika kuhamasisha wananchi kushiriki kwenye shughuli za usafi wa pamoja na kujenga utamaduni wa kutunza mazingira.

TTCL inaendelea kuchangia katika maendeleo endelevu ya jamii, kwa kuunganisha utoaji wa huduma za mawasiliano na shughuli za kijamii zinazolenga kuboresha ustawi wa wananchi na kuimarisha mahusiano kati ya Shirika, Serikali na jamii inayohudumiwa.