info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

TTCL YATUNUKIWA CHETI CHA PONGEZI KWA MCHANGO WAKE KATIKA KUFANIKISHA KONGAMANO LA MWAKA LA ANWANI ZA MAKAZI

Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limetunukiwa cheti maalumu cha pongezi na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kutambua mchango wake mkubwa katika kudhaminina kufanikisha Kongamano la Mwaka la Anwani za Makazi na Maonesho ya Teknolojia za Huduma za Posta.

Cheti hicho kilikabidhiwa na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angella Kairuki, wakati wa kilele cha kongamano hilo lililofanyika Februari 8, 2026, katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.

Awali Mhe. Kairuki alipongeza TTCL kwa hatua kubwa iliyofikiwa katika uunganishaji wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano katika Wilaya nyingi nchini, akieleza kuwa juhudi hizo zimekuwa nguzo muhimu katika kuboresha upatikanaji wa huduma za intaneti na mawasiliano ya kisasa.

Hata hivyo, Waziri Kairuki alilitaka shirika hilo kukamilisha uunganishaji wa Mkongo wa Taifa katika Wilaya 20 zilizosalia Tanzania Bara, sambamba na kuendelea kujitangaza zaidi ili wananchi na wadau mbalimbali wanufaike kikamilifu na huduma zinazotolewa na shirika hilo.

Cheti hicho kilipokelewa na Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa TTCL, Bw. Alex Biziriko, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo.

Kongamano la Anwani za Makazi na Maonesho ya Teknolojia za Huduma za Posta lilifanyika kwa muda wa siku nne kuanzia Februari 5 hadi 8, 2026, likiwa na kauli mbiu isemayo “Anwani Mahiri na Ubunifu wa Huduma za Posta kwa Ukuaji Jumuishi.”

Kongamano hilo liliwakutanisha wadau kutoka sekta mbalimbali za mawasiliano na teknolojia, likilenga kujadili fursa, changamoto na mikakati ya kutumia teknolojia za kisasa katika kuimarisha mifumo ya anwani za makazi na huduma za posta nchini.

Ushiriki wa TTCL katika kongamano hilo unaonesha dhamira ya dhati ya shirika hilo katika kuendelea kuwa mhimili wa maendeleo ya teknolojia ya mawasiliano na kuunga mkono juhudi za Serikali za kujenga uchumi wa kidijitali kwa ukuaji jumuishi na endelevu.