info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

TTCL YATUMIA SHIMMUTA 2026 KUTANGAZA HUDUMA NA KUIMARISHA UHUSIANO NA WATEJA

Na Adeline Berchimance

Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limeungana na Mashirika, Taasisi na Kampuni  mbalimbali za kiserikali katika uzinduzi wa Mashindano ya Michezo ya Mashirika, Taasisi na Makampuni (SHIMMUTA) 2026, yaliyofanyika katika Viwanja vya Jamhuri, mkoani Morogoro. 

Mashindano hayo yamezinduliwa rasmi na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mwigulu Chemba, yakilenga kuimarisha umoja, mshikamano na afya za wafanyakazi kupitia michezo.

Katika uzinduzi huo, wafanyakazi wa TTCL wameungana na wenzao kutoka taasisi na mashirika mbalimbali kushiriki katika hafla hiyo, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za kuendeleza michezo mahali pa kazi na kukuza mahusiano baina ya watumishi wa sekta mbalimbali nchini.

Mbali na kushiriki katika mashindano hayo, TTCL imetumia fursa ya SHIMMUTA 2026 kuimarisha shughuli zake za kibiashara na mawasiliano na umma kwa kukutana na wateja waliopo, kutafuta wateja wapya na kutangaza huduma mbalimbali za mawasiliano zinazotolewa na Shirika hilo.

Kupitia banda lake la maonyesho lililopo katika Viwanja vya Jamhuri Morogoro , TTCL inaendelea kutoa elimu kwa wananchi na washiriki wa mashindano kuhusu huduma zake mbalimbali, matumizi ya teknolojia za kisasa za mawasiliano na namna huduma hizo zinavyoweza kurahisisha shughuli za kijamii, kiuchumi na kibiashara.

Aidha, uwepo wa TTCL katika mashindano hayo ni sehemu ya mkakati wa Shirika wa kusogeza huduma karibu na wananchi, kuongeza uelewa kuhusu suluhisho za kidijitali na kujenga uhusiano wa karibu na wateja kupitia mawasiliano ya ana kwa ana. 

Fursa hii pia inawezesha TTCL kupata maoni na mahitaji ya wateja ili kuendelea kuboresha huduma zake kwa wananchi .

TTCL inawaalika wadau, wafanyakazi wa taasisi mbalimbali na washiriki wote wa SHIMMUTA 2026 kutembelea banda lake katika Viwanja vya Jamhuri, Morogoro, kujifunza na kujionea huduma mbalimbali zinazotolewa kwa ajili ya kuimarisha maendeleo kidigitali.