info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

TTCL YATOA WITO KWA WATUMISHI WAKE KUSHIRIKI MICHEZO KUIMARISHA AFYA NA MSHIKAMANO KAZINI

Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limeendelea kudhihirisha dhamira yake ya kuimarisha ustawi wa Watumishi wake kwa kuandaa Bonanza la Michezo lililofanyika Februari 14, mwaka huu katika Viwanja vya Posta Kijitonyama, jijini Dar es Salaam. 

Bonanza hilo liliwakutanisha Watumishi kutoka Mikoa ya Dar es Salaam, Makao makuu, Watumishi kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili pamoja na VIWA FC lengo likiwa ni kuimarisha afya, mshikamano na mahusiano ya kikazi.

Tukio hilo lilipambwa na michezo mbalimbali iliyochezwa kwa ushindani wa kirafiki, huku washiriki wakionesha ari, nidhamu na ushirikiano wa hali ya juu. Michezo iliyochezwa na ni pamoja na: Mpira wa Miguu, Mpira wa Pete, Mbio za Mita 100, Kukimbiza Kuku Kukimbia ndani ya Gunia, Kuvuta kamba, Draft, Karata, Mashindano ya Kula na Mchezo wa Bao 

Akizungumza wakati wa bonanza hilo, Mkurugenzi wa Fedha Bw. Straton Matei, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TTCL aliwapongeza watumishi wote kwa kujitokeza kwa wingi na kushiriki kikamilifu katika michezo mbalimbali, akisisitiza kuwa michezo ni nyenzo muhimu ya kuimarisha afya ya mwili na akili.

Matei aliipongeza Kamati ya maandalizi kwa kufanikisha tukio hilo, akibainisha kuwa michezo ni nyenzo muhimu ya kujenga nguvu kazi yenye afya, mshikamano na na kwamba afya bora kwa watumishi huchangia kuongeza ufanisi, weledi na ubora wa utendaji kazi.

Alisisitiza kuwa TTCL itaendelea kuunga mkono na kuhimiza shughuli za michezo ndani ya shirika, akieleza kuwa watumishi wenye afya njema na mahusiano mazuri ya kikazi ni msingi wa utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Katika kuhitimisha bonanza hilo, mgeni rasmi alikabidhi vikombe na midali kwa washiriki walioshinda katika michezo mbalimbali, huku akiwapongeza washiriki wote kwa kujitokeza na kushiriki kwa ari kubwa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Michezo Taifa, Bi Cecilia Medard, alisisitiza umuhimu wa michezo katika maisha ya watumishi na mafanikio ya Shirika ambapo alieleza kuwa michezo ina mchango mkubwa si tu katika kuboresha afya ya mwili na akili, bali pia katika kuimarisha umoja, nidhamu, ushirikiano na ari ya kufanya kazi kwa pamoja.

“Michezo ina nafasi kubwa sana katika maisha yetu ya kila siku. Mafanikio ya taasisi yoyote hutegemea kwa kiasi kikubwa mshikamano na ustawi wa wafanyakazi wake. Bonanza hili ni fursa muhimu ya kuimarisha mahusiano baina yetu, kujenga timu imara na kuongeza morali ya kazi,” alisema Bi Medard.

Aidha, aliishukuru Menejimenti ya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kwa kuendelea kuweka mazingira yanayochochea ustawi wa watumishi, huku akiwahimiza watumishi kuendeleza utamaduni wa kushiriki michezo kwa manufaa binafsi na kwa shirika kwa ujumla.