TTCL YATOA WITO KWA WADAU KUHAMIA UTALII WA KIDIGITALI
Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limetoa wito kwa wadau mbalimbali wa Utalii nchini kuhamia katika utalii wa kidigitali.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Masoko wa Shirika Bw. Vedastus Mwita kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu CPA Moremi Marwa katika Semina ya Wadau wa Utalii wa Tamasha la Swahili International Tourism Expo lililofanyika Oktoba, 2024 katika Ukumbi wa Mikutano wa Mlimani City Jijini Dar es salaam.
Bw. Mwita alisema kuwa Teknolojia ya utalii inakua kwa kasi kubwa hivyo ni vema sekta ya utalii kuendana na kasi hiyo kwa kuhamia katika utalii wa kidigitali kama njia ya kuvutia watalii wapya na kukuza utalii nchini.
Bw. Mwita alieleza kuwa teknolojia kama vile simu za mkononi, intaneti ya kasi na programu za simu zinaweza kutumika kuvutia utalii nchini ambapo alisema programu za simu zinasaidia watalii kupata taarifa kuhusu vivutio vya utalii, hoteli na huduma nyingine muhimu.
Akielezea faida kadhaa za utalii wa kidijitali, alisema kuwa utalii unatoa fursa kwa wajasiriamali wadogo kuanzisha biashara zao mtandaoni bila gharama kubwa, pili alisema inarahisisha upatikanaji wa taarifa sahihi kwa watumiaji ambao wanataka kupanga safari zao kwa urahisi zaidi.
Alibainisha kuwa TTCL itaendelea kuhimiza umuhimu wa uwekezaji katika teknolojia ya mawasiliano na elimu ili kukuza sekta ya utalii nchini.
Aidha alitoa wito kwa wadau kutoka sekta zote kushirikiana katika kuunda mfumo jumuishi unaotumia teknolojia ya mawasiliano ya simu kwa ukuaji endelevu wa utalii wa kidijitali.
Katika hatua nyingine Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limedhamini Maonesho ya Nane ya Utalii ya Swahili International Tourism Expo kwa kutoa intaneti ya bure yenye kasi wakati wote wa maonesho hayo lengo likiwa ni kuunga mkono juhudi za Serikali za kukuza utalii na kuvutia watalii kwa maendeleo endelevu ya nchi.