TTCL YATAMBULIWA KIMATAIFA KWA MCHANGO WAKE KATIKA MAENDELEO YA HUDUMA ZA FTTH TANZANIA
Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limeendelea kung'ara katika medani za kimataifa baada ya kutambuliwa kwa mara ya pili kwa mchango wake katika kuendeleza miundombinu ya mawasiliano ya Fiber to the Home (FTTH) nchini Tanzania.
Utambuzi huo umetolewa katika Kongamano la World Broadband Association (WBBA) Broadband Development Congress 2026, lililofanyika tarehe 16 Novemba 2026, jijini Cape Town, Afrika Kusini, ambapo TTCL imetunukiwa tuzo ya Gigacity Champion Award.
Katika kongamano hilo, Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Bw. Moremi Marwa, aliwasilisha mada kuhusu “Unlocking the Broadband Innovation for Tanzania's Digital Future”, akielezea mchango wa Shirika katika kuharakisha mageuzi ya kidijitali nchini kupitia uwekezaji wa miundombinu ya mawasiliano ya kisasa.
Katika wasilisho lake, Bw. Marwa alieleza mikakati ya TTCL ya kupanua huduma za FTTH, kuimarisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB), kuboresha uzoefu wa wateja kupitia teknolojia za akili bandia (AI), na kuongeza upatikanaji wa huduma za intaneti zenye kasi na ubora.
Aidha, alieleza dhamira ya TTCL ya kufikisha huduma za FTTH katika maeneo mengi zaidi nchini, ikiwemo mpango wa kufikia nyumba milioni moja kupitia miundombinu ya fiber katika kipindi cha miaka mitatu, ikiwa katika kipindi cha mwaka mmoja ujenzi ya maunganisho takribani 300,000 yakiwa yamekamilika.
Utambuzi huu wa kimataifa unaendelea kuimarisha nafasi ya TTCL kama mdau muhimu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Uchumi wa Kidijitali, huku Shirika likiendelea kuchangia upatikanaji wa huduma za mawasiliano, kukuza ubunifu na kuiwezesha Tanzania kuwa kitovu cha huduma za kidijitali katika Afrika Mashariki.