TTCL YASHIRIKI UZINDUZI WA MFUMO WA MTUMIAJI APP • Yaahidi kushirikiana kwa karibu na TCRA CCC
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Kairuki (Mb), amezindua Mfumo wa Kidijitali wa Kuhudumia Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano ujulikanao kama Mtumiaji App, ulioandaliwa na Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA CCC).
Hafla hiyo ilifanyika katika Ukumbi wa Millennium Tower jijini Dar es Salaam, ikiwakutanisha Wadau wa Sekta ya Mawasiliano pamoja na Wananchi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Waziri Kairuki alisema kuwa mfumo huo ni hatua muhimu katika kuboresha utoaji wa huduma za mawasiliano nchini na kwamba kupitia mfumo huo, watumiaji wataweza kupata taarifa muhimu ikiwemo elimu kuhusu matumizi sahihi ya huduma za mawasiliano pamoja na kuwasilisha changamoto na maoni yao kwa urahisi.
Aidha, Waziri Kairuki alibainisha kuwa Serikali inaendelea kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Uchumi wa Kidijitali wa mwaka 2024 hadi 2034 uliozinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo Mkakati huo unalenga kuongeza matumizi ya TEHAMA, kuimarisha uelewa wa kidijitali kwa wananchi na kuhakikisha huduma zinatolewa kwa wakati, kuongeza usalama na ufanisi.
Katika hafla hiyo Shirika la Mawasiliano Tanzania –TTCL lilikuwa miongoni mwa wadau muhimu katika sekta ya Mawasiliano nchini walioshiriki ambapo Mkurugenzi wa Fedha, Bw. Straton Matei, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, aliipongeza TCRA CCC kwa ubunifu wa kuanzisha mfumo huo akisema utasaidia kuimarisha mawasiliano kati ya watoa huduma na watumiaji.
Bw. Matei alisisitiza kuwa TTCL itaendelea kushirikiana kwa karibu na TCRA CCC katika kuboresha huduma kwa wateja na kuhakikisha maslahi ya wateja yanalindwa.
Katika kuonesha mchango wake katika kufanikisha tukio hilo, TTCL ilikabidhiwa tuzo maalum ya kutambua udhamini wake, ikiwa ni ishara ya kuthamini juhudi za shirika hilo katika kuunga mkono maendeleo ya sekta ya mawasiliano na ustawi wa watumiaji wake.
Aliongeza kuwa mfumo wa Mtumiaji App utakuwa jukwaa muhimu kwa watumiaji kupata elimu kuhusu matumizi sahihi ya huduma za mawasiliano, kutoa changamoto wanazokutana nazo pamoja na kupokea ushauri kwa urahisi kupitia teknolojia ya kidijitali, hatua itakayochangia kuongeza uwazi na uwajibikaji.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA CCC), Bi. Hawa Ngh’umbi, alisema mfumo huo utaleta mapinduzi katika namna watumiaji wa huduma za mawasiliano watakavyohudumiwa.
Alieleza kuwa kutokana na ongezeko la watumiaji wa simu linalozidi milioni 106 nchini, App hiyo itarahisisha utoaji wa huduma, kufuatilia changamoto zilizoripotiwa na kuhakikisha watumiaji wanapata majibu kwa haraka na kwa ufanisi zaidi.