
TTCL YASHIRIKI NA KUDHAMINI KIKAO KAZI CHA TATU CHA WENYEVITI WA BODI NA WAKUU WA TAASISI NA MASHIRIKA YA UMMA 2025
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Bw. Moremi Marwa, ameungana na Viongozi wengine wa Mashirika ya Umma kushiriki Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Umma kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Kikao hicho kilifunguliwa rasmi Agosti 24, 2025 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango, na kimebeba kaulimbiu muhimu inayosema: “Ushirikiano Endelevu wa Kibiashara katika Mazingira Shindani ya Kimataifa – Nafasi ya Mashirika ya Umma.”
Kaulimbiu hii imebeba ujumbe mpana kwa mashirika ya umma nchini, ikiweka msisitizo wa kuimarisha ubunifu, mshikamano na mikakati ya kibiashara inayoweza kuongeza tija na ufanisi.
Katika mazingira ya sasa ya ushindani wa kimataifa, mashirika ya umma ikiwemo TTCL yanakumbushwa kujiweka katika nafasi bora ya kibiashara kwa kujikita katika utoaji wa huduma zenye viwango vya kimataifa, ufanisi wa matumizi ya rasilimali, pamoja na kuongeza mchango katika pato la Taifa.
Kikao hiki kinajumuisha mashirika zaidi ya 300 na washiriki takribani 700 kutoka Taasisi, Mashirika ya Umma na Kampuni mbalimbali, jambo linaloonesha ukubwa na uzito wa dhana ya ushirikiano katika kukuza maendeleo ya Taifa.
Kupitia majadiliano na mikutano ya kitaalamu, washiriki wanatarajiwa kujadili changamoto, fursa na mikakati ya kuboresha usimamizi wa mashirika ya umma ili yaendelee kuwa chachu ya ukuaji wa uchumi wa nchi.
TTCL inashiriki katika kikao hiki kama jukwaa muhimu la kujifunza na kubadilishana uzoefu na mashirika mengine ya umma na pia shirika hilo linabeba jukumu kubwa katika kuunganisha wananchi, biashara na serikali kupitia kuwekeza katika teknolojia za kisasa zenye kutoa huduma bora na hivyo kuongeza nafasi yake katika ushindani wa Kikanda na Kimataifa.
Mbali na kushiriki, TTCL pia imekuwa mdhamini wa kikao hiki ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhakikisha taasisi za umma zinafanya kazi kwa ufanisi, uwajibikaji na ubunifu. Udhamini huu unaonesha dhamira ya shirika si tu kama mtoa huduma za mawasiliano, bali pia mshirika wa maendeleo ya kitaifa kupitia sekta ya TEHAMA.