TTCL YAPONGEZWA KWA MAGEUZI KIDIGITALI
Shirika la Mawasiliano Tanzania-TTCL limepongezwa kwa jitihada na kazi kubwa inayofanyika ya kuleta mageuzi kidijitali nchini.
Pongezi hizo zimetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Mkoani Mwanza Bw. Hassan Masalla wakati wa hafla ya kufuturisha Wafanyakazi na Wadau mbalimbali wa Sekta ya Mawasiliano Iliyofanyika Aprili 4, 2024 katika Hoteli ya Malaika jijini Mwanza.
Katika hafla hiyo iliyoandaliwa na Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL Bi. Zuhura Snare Muro, Bw. Masalla alipongeza juhudi zinazofanywa na serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania za kukuhakikisha wananchi wanapata huduma ya mawasiliano ili kurahisisha huduma za kiuchumi na kijamii.
Akizungumzia tendo la kufurisha, Bw. Masalla alisema TTCL kupitia kwa Mwenyekiti wake wa Bodi imefanya jambo jema kwani pamoja na mambo mengine tendo hilo linahimarisha na kujenga mahusiano mazuri na Wafanyakazi pamoja na wateja wao.
Alitoa pongezi kwa Mwenyekiti wa Bodi na Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Mhandisi Peter Ulanga kwa kuona umuhimu wa kufanya jambo hilo ambalo ni moja ya nguzo kuu katika dini ya Kiislam ambapo katika kipindi cha mfungo wa Ramadhani watu binafsi, Taasisi, Mashirika na Kampuni wanatumia kipindi hiki kutoa sadaka hasa kufuturisha makundi mbalimbali katika jamii.
“Nawapongeza sana kwakufanya jambo hili la kufuturisha na naomba niwaambieni hii imekuwa fursa nzuri kukutana na wadau wenu na kuimarisha upendo, umoja na mahusiano yenu na jamii mnayoihudumia” Amesema Masalla
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL, Bi Zuhura Sinare Muro aliwashukuru wote waliohudhuria katika hafla hiyo ya Iftari ambayo ni mara ya kwanza kufanyika nje ya Dar Es Salaam.
Alisema TTCL ni Shirika la Wananchi hivyo kwa muktadha huo Watumishi wa Shirika hilo wanapaswa kutambua kuwa wamebeba dhamana kubwa ya ulinzi na usalama wa nchi kupitia miundombinu ya Mawasiliano.
Alisema kila Mtumishi katika nafasi yake ahakikishe anaongeza bidii, ubunifu na uzalendo wa hali ya juu ili kuhakikisha huduma ya mawasiliano inapatikana kwakuzingatia ubora, urahisi na unafuu wa gharama.
Pia alimshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuliamini shirika hilo na kulipa dhamana ya kutunza na kuendesha miundombinu ya kimkakati ya mawasiliano na hivyo kuwataka Watumishi wa TTCL kutokumwangusha katika utekelezaji wa majukumu hayo makubwa waliyokabidhiwa.
kwamba kutuamini kwamba sisi TTCL ambao ni wazawa wa Mkongo katika Mawasiliano tubebe dhamana ya kuulinda.
"Tumebeba dhamana kubwa ya kulinda na kutunza miungombinu tuliyokabidhiwa kazi yetu kubwa ni kuhakikisha hatumwangushi Rais wetu na ahadi yetu ni kuwa jukumu hili tunalibeba kwa weledi wa hali ya juu”. Alisema Bi. Zuhura
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Mhandisi Peter Ulanga aliwashukuru wadau wote waliojumuika pamoja katika hafla hiyo ya Futari ambapo shirika limetumia fursa hiyo kukumbushana maagizo ambayo waumini wa dini ya Kiislam wamepewa na Mwenyezi Mungu kupitia mawaidha kutoka kwa Viongozi wao wa Dini
"Tumeipokea heshima kubwa ya kujumuika nasi na ni faraja kubwa sana kwetu" na kuongeza kuwa, Sisi kama Shirika la Mawasiliano tumeona ni vyema kutimiza maagizo ya Mwenyezi Mungu kwa kujumuika na Wadau wetu katika iftari ili kukumbushana maagizo mbalimbali ambayo tumeagizwa Mwenyezi Mungu.” Amesema Mhandisi Ulanga
Aidha katika hatua nyingine alitoa wito kwa Mashirika ya Umma, Taasisi binafsi na wabunifu katika masuala ya teknolojia kutumia fursa ya uwepo wa huduma ya Faiba Mlangoni Kwako kuboresha utendaji wao wa kazi na kuongeza ufanisi katika majukumu yao.