TTCL YAPOKEA WANAFUNZI WA ST. THERESE MAPINGA KWA ZIARA YA KIMAFUNZO
Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limepokea wanafunzi wa Shule ya Sekondari St. Therese Mapinga waliotembelea makao Makuu ya shirika kwa ziara ya mafunzo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa utafiti wao wa kitaaluma (Project Work) wenye mada isemayo, "The Role of TTCL Corporation in Improving Communication in Tanzania."
Ziara hiyo imelenga kuwapa wanafunzi uelewa wa kina kuhusu nafasi ya TTCL katika kuendeleza na kuboresha huduma za mawasiliano nchini, kupitia uwekezaji katika miundombinu ya TEHAMA, huduma za sauti, data, intaneti na suluhisho mbalimbali za kidijitali zinazochochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Katika ziara hiyo, wanafunzi walipata fursa ya kujifunza kuhusu historia ya Shirika, majukumu yake katika sekta ya mawasiliano, pamoja na mchango wake katika kuunga mkono ajenda ya Tanzania ya uchumi wa kidijitali. Aidha, walitembelea TTCL Museum ambapo walipata fursa ya kujifunza historia ya mawasiliano nchini Tanzania, kuona vifaa vya zamani na vya kisasa vya mawasiliano, na kufahamu hatua mbalimbali za maendeleo ya teknolojia ambazo zimeiwezesha Tanzania kuendelea kuimarisha huduma za mawasiliano kwa wananchi.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Afisa Uhusiano Mwandamizi wa TTCL Bw. Edwin Mashasi alisema shirika linaendelea kuthamini ushirikiano na taasisi za elimu kwa kuwawezesha wanafunzi kujifunza kwa vitendo na kupata uelewa mpana kuhusu sekta ya mawasiliano na teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA).
Kwa upande wao, wanafunzi wa Shule ya Sekondari St. Therese Mapinga walieleza shukrani zao kwa TTCL kwa kuwapatia fursa ya kujifunza kwa vitendo, wakieleza kuwa maarifa waliyoyapata yatawasaidia kukamilisha utafiti wao na kuongeza uelewa kuhusu mchango wa TTCL katika kuboresha mawasiliano nchini Tanzania.
Shirika la Mawasiliano Tanzania litaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali za elimu katika kukuza maarifa, ubunifu na matumizi ya teknolojia kwa maendeleo endelevu ya Taifa na ujenzi wa uchumi wa kidijitali.