TTCL YAONGEZA KASI YA UPANUZI WA HUDUMA ZA FAIBA ARUSHA, MKURUGENZI MKUU AKAGUA MAENDELEO
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Bw. Moremi Marwa, amefanya ziara ya kukagua maendeleo ya utoaji wa huduma ya intaneti yenye kasi ya TTCL Faiba katika makazi ya wananchi jijini Arusha, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Shirika za kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora, za uhakika na zenye kukidhi mahitaji ya uchumi wa kidijitali.
Katika ziara hiyo, Bw. Marwa alitembelea Kata ya Moshono, moja ya maeneo ambayo tayari yameunganishwa na huduma ya TTCL Faiba. Huduma hiyo pia inapatikana katika kata za Themi, Engutoto na Baraa, ambapo wananchi wanaendelea kunufaika na huduma za intaneti zenye kasi na ubora wa hali ya juu.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkurugenzi Mkuu alisisitiza umuhimu wa kuendelea kupanua upatikanaji wa huduma za kidijitali kwa wananchi ili kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi, kuongeza fursa za biashara na kuboresha utoaji wa huduma mbalimbali zinazotegemea teknolojia.
““Ongezeni juhudi za kukuza biashara katika mji wa Karatu kwa kusajili wateja wengi zaidi, kuimarisha huduma kwa wateja, na kuhakikisha inaendelea kuwa chaguo bora la huduma za mawasiliano aidha, TTCL itaendelea kuwekeza katika upanuzi wa miundombinu ya mawasiliano ili kuhakikisha huduma za kisasa za intaneti zinawafikia Watanzania wengi zaidi na kuchangia katika ujenzi wa uchumi wa kidijitali,” alisema Bw. Marwa.
Katika hatua nyingine ya ziara hiyo, Mkurugenzi Mkuu alikagua maendeleo ya miundombinu ya mawasiliano iliyojengwa katika Uwanja wa AFCON Arusha, ambapo TTCL imekamilisha ujenzi wa miundombinu ya Mkongo wa Mawasiliano kwa lengo la kuimarisha huduma za mawasiliano katika uwanja huo utakaotumika kwa mashindano ya AFCON.
Bw. Marwa alisema TTCL imejipanga kuhakikisha huduma za mawasiliano zinapatikana kwa uhakika wakati wote katika uwanja huo ili kuwezesha mawasiliano bora kwa waandaaji, washiriki, wadau na mashabiki kabla, wakati na baada ya mashindano.
Aidha, alibainisha kuwa kukamilika kwa miundombinu hiyo ni kielelezo cha dhamira ya TTCL ya kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuimarisha miundombinu ya mawasiliano nchini na kuwezesha Tanzania kuwa kitovu cha huduma za kidijitali na mawasiliano katika ukanda wa Afrika Mashariki.