TTCL YANG’ARA KIMATAIFA, YATWAA TUZO YA UBORA WA UTEKELEZAJI WA MIUNDOMBINU YA FAIBA MLANGONI KWAKO
Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limeendelea kuandika historia katika sekta ya mawasiliano baada ya kutunukiwa tuzo ya kimataifa ya “Best Application of FTTH Construction”, inayotambua ubora wa utekelezaji wa miundombinu ya intaneti ya kasi kupitia teknolojia ya Fibre to the Home (FTTH).
Tuzo hiyo imetolewa katika Jukwaa la Kimataifa la Ultra-Broadband (UBBF) 2026, lililofanyika jijini Vienna, Austria, kuanzia Oktoba 12 hadi 14, 2026, likiwakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya mawasiliano duniani kujadili maendeleo ya teknolojia na mustakabali wa huduma za intaneti ya kasi.
Jukwaa hilo limeandaliwa kwa ushirikiano kati ya kampuni ya Huawei na Chama cha Kimataifa cha Broadband (World Broadband Association – WBBA), sambamba na tukio la kimataifa la Network X.
Chini ya kaulimbiu “Agentic UBB, Beyond Connectivity”, jukwaa hilo limejikita katika kujadili namna teknolojia za intaneti ya kasi, mifumo mahiri na matumizi ya Akili Unde (Artificial Intelligence – AI) zinavyoweza kuleta mageuzi katika utoaji wa huduma za mawasiliano, kuongeza ufanisi, kuchochea ubunifu na kufungua fursa mpya za kiuchumi na kijamii.
Kutunukiwa kwa tuzo hiyo ni hatua muhimu kwa TTCL katika utekelezaji wa mkakati wake wa kupanua huduma za intaneti ya kasi kupitia Faiba Mlangoni Kwako, inayolenga kuongeza upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa wananchi, taasisi na wafanyabiashara nchini.
Katika mwaka 2026, TTCL imefanikiwa kusambaza miundombinu ya FTTH inayofikia nyumba 280,000 (Homes Passed), hatua inayoongeza uwezekano wa wananchi wengi zaidi kuunganishwa na huduma ya intaneti ya kasi katika maeneo yaliyofikiwa na miundombinu hiyo.
Upanuzi huo unatoa fursa kwa familia kutumia huduma za kusoma mtandaoni, burudani, kuwawezesha wananchi kufanya kazi kwa njia ya kidijitali, pamoja na kusaidia wafanyabiashara na taasisi kutumia teknolojia kuongeza ufanisi na tija katika shughuli zao.
Tuzo hii ya kimataifa inaendelea kuimarisha nafasi ya TTCL katika sekta ya mawasiliano na kuonesha maendeleo ya Shirika katika utekelezaji wa miundombinu ya kisasa inayokidhi mahitaji yanayoongezeka ya huduma za intaneti ya kasi.
Aidha, mafanikio hayo yanadhihirisha mchango wa TTCL katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kuharakisha mageuzi ya kidijitali, kupanua matumizi ya TEHAMA na kuweka mazingira wezeshi kwa maendeleo ya uchumi wa kidijitali nchini Tanzania.
TTCL itaendelea kuwekeza katika upanuzi na uboreshaji wa miundombinu ya mawasiliano, kuimarisha ubora wa huduma na kusogeza intaneti ya kasi karibu zaidi na wananchi, ili kuwawezesha Watanzania kunufaika na fursa zinazotokana na maendeleo ya teknolojia.