TTCL YAJIPANGA KIKAMILIFU KUWAHUDUMIA WATEJA SABASABA 2026
Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limejipanga kikamilifu kuhakikisha wateja na wananchi wanaotembelea Banda Na. 26 katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba 2026) wanapata huduma bora, elimu kuhusu bidhaa na huduma mbalimbali za kidijitali, pamoja na suluhisho zinazokidhi mahitaji yao.
Katika kipindi chote cha maonesho yanayofanyika kuanzia Juni 28 hadi Julai 13, 2026 katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Sabasaba, TTCL imeweka timu ya wataalamu kutoka idara mbalimbali ili kutoa huduma za ushauri, usajili wa huduma na majibu ya papo kwa papo kwa wateja.
Wageni wanaotembelea banda la TTCL wanapata fursa ya kujionea na kupata huduma mbalimbali zikiwemo Faiba Mlangoni Kwako (FTTH), huduma za simu za mkononi, T-PESA, Cloud Computing, FTTx Experience Centre, huduma za Call Centre, pamoja na suluhisho nyingine za TEHAMA zinazolenga kuboresha mawasiliano kwa watu binafsi, taasisi na wafanyabiashara.
Aidha, TTCL inatoa huduma TTCL Public Wi-Fi ndani ya banda lake, huku wataalamu wa Shirika wakitoa elimu kuhusu matumizi ya huduma za kidijitali na namna zinavyoweza kuongeza ufanisi katika shughuli za kila siku.
Ili kuongeza thamani kwa wateja, TTCL imeandaa ofa maalum za Sabasaba, zinazojumuisha punguzo la bei za modem na router, pamoja na fursa ya kujisajili na kuanza kutumia huduma mbalimbali za Shirika papo kwa papo.
Akizungumzia maandalizi hayo, Meneja wa Banda Bi.Janeth Maeda ameeleza kuwa ushiriki wa TTCL katika maonesho hayo ni sehemu ya mkakati wa kusogeza huduma karibu na wananchi, kusikiliza mahitaji ya wateja na kuendelea kutoa suluhisho bunifu za mawasiliano na teknolojia ya habari.
TTCL inawakaribisha wateja, wadau na wananchi wote kutembelea Banda Na. 26 ili kujionea teknolojia za kisasa, kupata huduma kutoka kwa wataalamu wa Shirika na kunufaika na ofa mbalimbali zinazotolewa wakati wa maonesho.