TTCL YAIMARISHA NAFASI YA TANZANIA KUWA KITOVU CHA MAWASILIANO NA FURSA ZA KIDIJITALI UKANDA WA MAZIWA MAKUU
Na Spencer Julius
Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limeendelea kuimarisha nafasi ya Tanzania kupitia Mkoa wa Kigoma katika ramani ya mawasiliano ya kikanda kupitia uwekezaji wa kimkakati katika miundombinu ya mawasiliano, hatua inayolenga kuunganisha Tanzania na nchi Jirani ya Kongo pamoja na kuongeza upatikanaji wa huduma za intaneti ya kasi kwa wananchi.
Katika kuendeleza dhamira hiyo, Wajumbe wa Bodi ya TTCL, wakiongozwa na Prof. Saudin Jacob Mwakaje, wamefanya ziara katika mkoa wa Kigoma kwa lengo la kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya mawasiliano wa ujenzi wa kituo cha makutano ya miundombinu ya mkongo wa mawasiliano unaounganisha Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kupitia Ziwa Tanganyika, Kigoma.
Mradi huo ni sehemu ya juhudi za TTCL katika kuimarisha muunganisho wa mawasiliano wa kikanda utakaofanya Kigoma kuwa eneo muhimu la kimkakati katika huduma za mawasiliano kati ya Tanzania na nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu.
Katika hatua nyingine, Wajumbe wa Bodi ilitembelea na kukagua utekelezaji wa mradi wa Faiba Mlangoni Kwako (FTTH) Awamu ya Pili, ambao tayari ujenzi wa miundombinu yake umeanza katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Kigoma.
Mradi huu unalenga kusogeza huduma za intaneti ya kasi moja kwa moja kwa wananchi kupitia teknolojia ya nyuzi za kisasa (Fiber Optic), utakaowezesha kaya, wafanyabiashara, taasisi za elimu, vituo vya afya na ofisi za umma kupata huduma za mawasiliano zenye kasi, uhakika na ubora wa juu.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Wajumbe ya TTCL, Prof. Saudin Jacob Mwakaje, amesisitiza umuhimu wa miradi hiyo katika kutekeleza dhamira ya Shirika ya kuhakikisha miundombinu ya mawasiliano inakuwa kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi na kijamii.