info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

TTCL YAENDELEA NA MAGEUZI YA KIDIJITALI: YASHIRIKI WARSHA YA KIMATAIFA YA TEKNOLOJIA ILIYOANDALIWA NA KAMPUNI YA NOKIA

Timu ya wataalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kutoka Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), ikiongozwa na Mkurugenzi wa Ufundi Mhandisi Cecil Francis, imeungana na Wadau wengine wa Teknolojia Duniani katika Warsha Maalum ya Kimataifa iliyoandaliwa na Kampuni ya Nokia na kufanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency, jijini Dar es Salaam hivi karibuni.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Mhandisi Cecil alieleza kuwa TTCL inaendelea kuwa kiungo muhimu katika safari ya mageuzi ya kidijitali hapa nchini. 

Mhandisi Cecil alisisitiza kuwa ushiriki wa TTCL katika warsha hiyo ni hatua madhubuti ya kuongeza uwezo wa kitaalamu, kuboresha mikakati ya kiteknolojia na kukuza ushirikiano wa Kimataifa unaolenga kuharakisha upatikanaji wa huduma bora za mawasiliano kwa Watanzania.

Warsha hiyo ilibeba mada mbalimbali muhimu zenye lengo la kuchochea kasi ya maendeleo ya kidijitali nchini pamoja na ajenda mbalimbali ikiwemo  tathmini ya mazingira ya soko la mawasiliano nchini, mchango wa Nokia katika kusaidia mashirika kufikia malengo yao ya kidijitali, na mwenendo wa kimataifa wa huduma za intaneti ya waya (Fixed Broadband).

Aidha, mada nyingine zilizojadiliwa ni pamoja na mageuzi ya teknolojia ya BNG Routers kupitia mifumo ya kisasa ya MAG/SDWAN, uboreshaji wa majukwaa ya uchanganuzi kuelekea IXR, thamani ya suluhisho za NSP na CARE, pamoja na mkakati wa Nokia wa kuendeleza vituo vya data duniani kwa lengo la kujenga mitandao iliyo ya kasi, thabiti, na yenye uwezo wa kujifunza kimtandao (smart networks).

Warsha hii imekuwa fursa kwa Wataalamu wa TTCL kujifunza,kujenga ushirikiano na kuongeza uelewa wa kutumia teknolojia za kisasa kuhakikisha Tanzania inanufaika kikamilifu na fursa za dunia ya kidijitali.