info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

TTCL YAENDELEA KUWEKEZA KATIKA KIZAZI KIJACHO CHA WAHANDISI WA MAWASILIANO NCHINI

Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limeendelea kuonesha dhamira yake ya kuwekeza katika maendeleo ya rasilimali watu na kukuza kizazi kijacho cha wataalamu wa mawasiliano nchini kwa kuwapokea wanafunzi kutoka Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), waliotembelea Makao Makuu ya Shirika jijini Dar es Salaam kwa mafunzo ya vitendo yaliyofanyika tarehe 30–31 Julai 2026.

 

Wanafunzi hao, wakiambatana na wakufunzi wao, walipata fursa ya kujifunza kwa vitendo shughuli mbalimbali za kiufundi na kiutendaji zinazotekelezwa na TTCL, hatua inayolenga kuwajengea ujuzi wa kitaalamu, uzoefu wa moja kwa moja katika sekta ya mawasiliano na kuwaandaa kwa mahitaji ya soko la ajira la sasa na la baadaye.

 

Mafunzo hayo yalitoa nafasi kwa wanafunzi kuelewa historia na mageuzi ya TTCL tangu kuanzishwa kwake hadi kufikia hatua ya sasa kama mwezeshaji mkuu wa miundombinu ya mawasiliano na huduma za kidijitali nchini. Aidha, walitembelea Kituo cha Uendeshaji wa Mtandao ambapo walijionea namna mifumo ya mawasiliano inavyofuatiliwa na kusimamiwa ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora na endelevu kwa wateja nchini kote.

 

Hatua hii inaendana na mkakati wa TTCL wa kukuza wataalamu wenye ujuzi wa kisasa katika nyanja za mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), sambamba na jukumu lake la kuendelea kuwezesha mawasiliano ya kidijitali kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, unaounganisha huduma za mawasiliano katika maeneo mbalimbali ya Tanzania.

 

TTCL inaamini kuwa ushirikiano wa karibu na taasisi za elimu ya juu ni msingi muhimu wa kuibua vipaji vya kitaifa, kuimarisha ubunifu na tafiti, pamoja na kuandaa kizazi kipya cha wahandisi na wataalamu wa TEHAMA watakaosaidia kuendeleza uchumi wa kidijitali wa Tanzania.

 

Kupitia programu za mafunzo kwa vitendo na ushirikiano wa kitaaluma, TTCL itaendelea kushiriki kikamilifu katika juhudi za Taifa za kujenga nguvu kazi yenye ujuzi, weledi na uwezo wa kuendesha mapinduzi ya kidijitali nchini.