info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

TTCL YAENDELEA KUTOA HUDUMA NA ELIMU KWA WANANCHI SABASABA 2026

Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) linaendelea kutumia Maonesho ya 50 ya Biashara ya  Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba 2026) kutoa huduma na elimu kwa wananchi kuhusu bidhaa na huduma mbalimbali za mawasiliano zinazotolewa na Shirika hilo.

Maonesho hayo yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius K. Nyerere, Sabasaba, jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 28 Juni hadi 13 Julai 2026, yameendelea kuwa jukwaa muhimu kwa TTCL kuimarisha ukaribu na wateja, kupokea maoni yao na kuwapatia suluhisho mbalimbali za mawasiliano zinazokidhi mahitaji yao.

Katika Banda la TTCL, wananchi wanaendelea kupata elimu kuhusu huduma za intaneti ya kasi ya Faiba, huduma za sauti, data, Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano pamoja na suluhisho mbalimbali za TEHAMA zinazotolewa kwa wateja binafsi, taasisi za umma na sekta binafsi.

Mbali na kutoa elimu, wataalamu wa TTCL wanaendelea kutoa huduma kwa wateja papo kwa papo ikiwemo usajili wa huduma, kutoa ushauri wa kitaalamu, kushughulikia changamoto mbalimbali za wateja na kuelekeza wananchi kuchagua huduma zinazokidhi mahitaji yao.

Wananchi wanaotembelea banda hilo pia wanapata fursa ya kujifunza kuhusu maendeleo ya Shirika katika kuimarisha miundombinu ya mawasiliano nchini, matumizi ya teknolojia za kisasa na mchango wa TTCL katika kuendeleza uchumi wa kidijitali na utekelezaji wa ajenda ya Tanzania ya Kidijitali.

Akizungumza katika maonesho hayo, mmoja wa maafisa wa TTCL alisema ushiriki wa Shirika katika Sabasaba 2026 unalenga kuwasogezea wananchi huduma, kuongeza uelewa kuhusu bidhaa na huduma zinazotolewa na TTCL, pamoja na kujenga mahusiano imara na wateja na wadau mbalimbali.

Aidha, alibainisha kuwa maonesho hayo yanatoa fursa kwa Shirika kupokea mrejesho wa wateja ili kuendelea kuboresha huduma na kuendana na mahitaji ya soko la mawasiliano linalobadilika kwa kasi.

TTCL inaendelea kuwakaribisha wananchi kutembelea Banda la Shirika katika Maonesho ya Sabasaba 2026 ili kujionea huduma mbalimbali, kupata ushauri wa kitaalamu na kufahamu suluhisho za mawasiliano na TEHAMA zinazochangia maendeleo ya wananchi, taasisi na Taifa kwa ujumla.