info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

TTCL YAENDELEA KUSOGEZA HUDUMA ZA KIDIJITALI KARIBU NA WANANCHI

Na Adeline Berchmance

Mkurugenzi wa Biashara wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL Bw. Vedastus Mwita ameshiriki katika kipindi cha Baragumu Live cha televisheni kupitia Channel Ten na kueleza hatua mbalimbali zinazotekelezwa na Shirika katika kuimarisha na kupanua huduma za mawasiliano ya kidijitali nchini.

Akizungumza katika kipindi hicho, Bw. Mwita ameeleza kuhusu huduma ya Faiba Mlangoni Kwako (FTTH), ikiwa na lengo la kuwawezesha wananchi, familia, taasisi na wafanyabiashara kupata muunganisho unaokidhi mahitaji yao ya kidijitali.

Katika kipindi hicho, imeelezwa kuwa TTCL inaendelea kutekeleza Awamu ya Pili ya upanuzi wa miundombinu ya Faiba Mlangoni Kwako, kwa lengo la kuongeza maeneo yanayoweza kufikiwa na huduma ya intaneti ya kasi.

Upanuzi huo unalenga kuwawezesha wananchi, taasisi na wafanyabiashara wengi zaidi kupata huduma na kutumia fursa mbalimbali zinazotokana na maendeleo ya teknolojia na uchumi wa kidijitali.

Mkurugenzi wa Biashara pia ameeleza kuhusu teknolojia ya Fiber to the Room (FTTR), ambayo inalenga kuboresha usambazaji wa muunganisho ndani ya nyumba au jengo hadi katika vyumba na maeneo mbalimbali. Teknolojia hiyo inaweza kuwa na manufaa hususan katika nyumba kubwa au zenye vyumba vingi ambako baadhi ya maeneo yanaweza kuwa na signal dhaifu.

Katika kuendelea kuongeza thamani kwa wateja wa Faiba Mlangoni Kwako, amezungumzia pia T-Burudani Plus, huduma ya burudani ya kidijitali inayowawezesha wateja wenye huduma hai ya TTCL FTTH kupata maudhui mbalimbali, yakiwemo Live TV na Video on Demand.

Kwa mujibu wa masharti ya huduma, T-Burudani Plus imejumuishwa kama manufaa ya ziada kwa mteja mwenye huduma hai ya FTTH bila gharama nyingine ya usajili wa huduma hiyo.

Akizungumzia nafasi ya TTCL katika mageuzi ya kidijitali nchini, Bw Mwita ameeleza kuwa uwekezaji na upanuzi wa miundombinu ya faiba unalenga kuongeza muunganisho wa kidijitali na kuwawezesha wananchi, taasisi na wafanyabiashara kutumia teknolojia katika shughuli zao za kila siku.

Kuongezeka kwa muunganisho kunapanua fursa za matumizi ya teknolojia katika elimu, biashara, kazi, mawasiliano na huduma mbalimbali za kidijitali, na hivyo kuongeza ushiriki katika uchumi wa kidijitali.

Aidha, wananchi wamehimizwa kuwasiliana na TTCL kupitia njia rasmi ili kufahamu kama maeneo yao yamefikiwa na Faiba Mlangoni Kwako na kupata maelekezo ya namna ya kuomba huduma.