info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

TTCL YADHAMINI KONGAMANO LA NANE LA TEHAMA 2024

Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limeendelea kudhihirisha umuhimu wake katika sekta ya mawasiliano nchini kwa kushiriki kikamilifu katika Kongamano la Nane la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) lililofanyika mwaka 2024. 

Kongamano hili la siku tano limewaleta pamoja wataalamu, watoa maamuzi, na wadau mbalimbali wa teknolojia kutoka ndani na nje ya nchi limefanyika katika Ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam ambalo lililenga kujadili masuala ya ubunifu, ukuaji wa TEHAMA, na ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi katika kuendeleza uchumi wa kidijitali nchini.

Kongamano hilo lilifunguliwa rasmi na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Silaa (Mb) likiwa na kaulimbiu ya "Kutumia Uwezo wa Akili Mnemba na Robotiki kwa Mapinduzi ya Kiuchumi na Kijamii". 

Katika uzinduzi wa kongamano hilo Waziri Slaa aliambatana na Mhe. Merryprisca Mahundi (Mb) Naibu Waziri wa Habari, Mawasilianao na Teknolojia ya Habari pamoja na Bw, Mohammed Khamis Abdulla, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo

Akihutubia washiriki wa kongamano hilo Waziri Silaa aligusia umuhimu wa kongamano hili katika kuendeleza sekta ya TEHAMA nchini, huku akisisitiza umuhimu wa kutumia teknolojia ya kisasa kama vile Akili Mnemba na Robotiki katika kuleta mabadiliko chanya katika uchumi na jamii zetu. 

Katika kongamano hili, TTCL kupitia banda lake la maonesho ilipata fursa ya kuonesha huduma na bidhaa zake zinazolenga kuboresha huduma za mawasiliano na ukuaji wa matumizi ya TEHAMA katika sekta mbalimbali ikiwa ni pamoja na biashara, kilimo, elimu na afya. 

Aidha Washiriki wakongamano hilo kupitia banda la TTCL walioneshwa jinsi Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ulivyo leta mapinduzi ya upatikanaji wa huduma kidigitali kwa wananchi kwa haraka kupita matumizi ya TEHAMA baada ya miundo mbinu hiyo kuunganishwa katika Mikoa, Wilaya, nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na jinsi Data Center ilivyo chachu ya kuhifadhi kumbukumbu kimtandao kwa Kampuni, Mashirika, Taasisi za ndani na nje.

Katika hatua nyingine Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kama mdau muhimu katika kongamano hilo lilidhamini utekelezaji wa kongamano hilo kwakutoa huduma ya intaneti ya Wi-Fi ili kuwawezesha washiriki kuwa na uwezo wa kupata huduma ya intaneti yenye uhakika na ubora unaoendana na mabadiliko ya teknolojia ya mawasiliano kwa sasa.

Udhamini huu ulilenga kuhakikisha kikao hicho kinafanyika bila changamoto huku washiriki wakipata fursa ya kutumia mtandao wa kuaminika kwa ajili ya mawasiliano na uwasilishwaji wa taarifa za kikao hicho.

Aidha utekelezaji wa huduma hii ya Intaneti, ni sehemu ya mpango mkakati wa Shirika katika kuhakikisha maeneo yote muhimu ya umma na yale ya kimkakati yanawezeshwa na huduma za intaneti yenye kasi kwa matumizi ya wananchi wote kwa ujumla.

Hivi sasa, Shirika tayari limetekeleza mradi wa interneti ya umma "public WiFi" katika vyuo vya IFM, IAA, SUA, UDSM-CoICT, vituo vya SGR na Mlima kilimanjaro katika vituo vyote mpaka kileleni.

Kongamano la Nane la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) 2024 limekuwa jukwaa muhimu kwa TTCL kushirikiana na wadau wa sekta ya teknolojia na kuimarisha nafasi yake kama mtoa huduma wa mawasiliano anayejali mahitaji ya Watanzania na kuweka mbele ustawi wa Taifa.