info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

TTCL YADHAMINI JUKWAA LA SATELAITI LA SADC, YATOA INTANETI YA BURE KWA WASHIRIKI

Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limeendelea kuthibitisha nafasi yake muhimu katika kukuza sekta ya mawasiliano nchini na ukanda wa Kusini mwa Afrika kwa kushiriki kikamilifu katika Jukwaa la Pamoja la Satelaiti la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), linalofanyika kuanzia tarehe 16 hadi 20, Februari 2026 katika Ukumbi wa Johari Rotana, jijini Dar es Salaam. 

Kupitia udhamini huo, Shirika hilo limetoa huduma ya Intaneti likilenga kuwezesha washiriki na wadau mbalimbali kupata mawasiliano ya uhakika katika kipindi chote cha mkutano huo ili kuongeza ufanisi wa mawasiliano, kurahisisha upatikanaji wa taarifa na ushiriki mpana katika mijadala ya kitaalamu.

Jukwaa hilo limewakutanisha Wataalam wa Mawasiliano, Wabunifu wa Teknolojia, Watunga Sera na Wadau wa Sekta ya Anga za juu kutoka Nchi 16 Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), pamoja na Taasisi za Kikanda na Kimataifa likiwa na lengo la kujadili maendeleo ya teknolojia za satelaiti na mchango wake katika kuharakisha uchumi wa kidijitali na kuimarisha miundombinu ya mawasiliano katika Ukanda wa SADC.

Akifungua rasmi jukwaa hilo, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari (Mb), Angellah Jasmine Kairuki, alisisitiza umuhimu wa nchi wanachama kutumia teknolojia za kisasa ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya kidijitali duniani. 

Alieleza kuwa Tanzania itaendelea kuimarisha huduma za mawasiliano kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, kama sehemu ya juhudi za kukuza uchumi wa kidijitali wa Kikanda.

Mbali na mchango wake katika jukwaa hilo, TTCL imeendelea kusambaza huduma ya intaneti ya Umma katika maeneo ya kimkakati, ikiwemo Taasisi za Elimu ya Juu kama Institute of Finance Management (IFM), Institute of Accountancy Arusha (IAA), Sokoine University of Agriculture (SUA) na UDSM–CoICT.

Huduma hiyo pia imefikishwa katika vituo vya Reli ya kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR) na katika Mlima Kilimanjaro hadi kufikia kilele chake, hatua zinazoendelea kupanua wigo wa mawasiliano, upatikanaji wa intaneti nchini na kuimarisha uchumi.