TTCL YADHAMINI HUDUMA YA INTANETI KATIKA KONGAMANO LA KWANZA LA KITAIFA LA FARAGHA NA ULINZI WA TAARIFA BINAFSI 2026
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Dkt. Switbert Zacharia Mkama (Mb), amefungua rasmi Kongamano la Kwanza la Kitaifa la Faragha na Ulinzi wa Taarifa Binafsi 2026, linalofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam, kuanzia Juni 29 hadi Julai 1, 2026.
Akifungua kongamano hilo, Mhe. Dkt. Mkama alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya taasisi za umma na binafsi katika kuhakikisha taarifa binafsi za wananchi zinalindwa kwa kuzingatia sheria, maadili na matumizi salama ya teknolojia za kidijitali.
"Ni vyema kuwa na kongamano rasmi la masuala ya faragha na ulinzi wa taarifa binafsi kwa lengo la kukutana kwa pamoja na kujadiliana masuala muhimu yanayohusu faragha na ulinzi wa taarifa binafsi, na kuwa na mwelekeo wa pamoja kama taifa," amesema Mhe. Dkt. Mkama.
Katika kongamano hilo, Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) linajivunia kuwa miongoni mwa wadhamini kwa kutoa huduma ya intaneti ya kasi na uhakika, inayowawezesha washiriki kufuatilia na kushiriki kikamilifu mijadala, mawasilisho na shughuli zote za kongamano bila vikwazo vya mawasiliano.
Mbali na udhamini huo, watumishi wa TTCL wanashiriki kikamilifu katika kongamano hilo kwa kufuatilia mijadala ya kitaalamu na kubadilishana uzoefu na wadau mbalimbali kuhusu ulinzi wa taarifa binafsi, usalama wa mifumo ya TEHAMA, usimamizi wa data na maendeleo ya teknolojia za mawasiliano katika mazingira ya kidijitali.
Kongamano hilo limewakutanisha wadau kutoka sekta za umma na binafsi, wataalamu wa TEHAMA, wasimamizi wa sheria, taasisi za udhibiti pamoja na washirika wa maendeleo, kwa lengo la kujadili changamoto, fursa na mikakati ya kuimarisha faragha na ulinzi wa taarifa binafsi nchini katika enzi ya mageuzi ya kidijitali.
Ushiriki wa TTCL katika kongamano hili unaakisi dhamira ya Shirika ya kuendelea kusaidia maendeleo ya uchumi wa kidijitali kwa kutoa miundombinu na huduma za mawasiliano zilizo salama, za kuaminika na zenye ubora, sambamba na kuunga mkono juhudi za Serikali za kujenga Tanzania salama, iliyounganishwa na inayoendeshwa na teknolojia za kisasa.
#TTCL
#UlinziWaTaarifaBinafsi
#DataProtection
#DigitalTransformation
#TanzaniaDigital