info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

TTCL YAANZISHA FTTH CLINIC CENTERS KUREJESHA HUDUMA NA KUIMARISHA UAMINIFU WA WATEJA

Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limeanzisha mpango wa FTTH Clinic Centers unaolenga kurejesha huduma kwa wateja wa Faiba Mlangoni Kwako walioathirika na changamoto za kiufundi, sambamba na kuimarisha uaminifu, kuridhika na uzoefu wa wateja katika matumizi ya huduma za intaneti ya kasi.

Kupitia mpango huo, TTCL inalenga kuwafikia wateja ambao huduma zao zimekatika au kusitishwa kutokana na changamoto mbalimbali, kwa kufanya uchunguzi wa hitilafu, kutoa usaidizi wa kitaalamu na kuhakikisha changamoto hizo zinapatiwa ufumbuzi kwa ufanisi.

Akizungumza wakati wa mafunzo kuhusu utekelezaji wa mpango huo, Bw. Mohamed Shaban amesisitiza umuhimu wa kushughulikia changamoto za wateja ili kuhakikisha wanaendelea kupata huduma bora na za uhakika.

“Kupitia FTTH Clinic Centers tunalenga kutoa huduma kwa mteja kwa kuhakikisha tunashughulikia changamoto zote zilizojitokeza ili mteja aendelee kupata uzoefu bora wa huduma,” amesema Bw. Shaban.

Mpango huo unatekelezwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya na Dodoma ikiwa ni sehemu ya juhudi za kimkakati za Shirika katika kuimarisha huduma kwa wateja, kurejesha wateja waliositisha matumizi ya huduma na kujenga mahusiano endelevu kati ya Shirika na wateja wake.

Kuanzishwa kwa FTTH Clinic Centers ni katika kuendeleza mikakati ya kuhakikisha changamoto zinazowakabili wateja zinapatiwa ufumbuzi na kuwawezesha kuendelea kufurahia huduma za intaneti ya kasi, zenye ubora, uhakika na zinazokidhi mahitaji ya ulimwengu wa kidijitali.