info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

TTCL YAANDIKA HISTORIA, YATUNUKIWA TUZO NA RAIS SAMIA BAADA YA KUREJEA KWENYE FAIDA

Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limeandika historia mpya baada ya kutunukiwa Tuzo Maalum na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kufuatia mafanikio ya kurejea kwenye faida kwa mara ya kwanza baada ya kipindi kirefu cha changamoto za kifedha.

TTCL imepata faida ya Shilingi bilioni 22.9 katika mwaka wa fedha uliopita na kutoa gawio la Shilingi bilioni 1.6 kwa Serikali, mafanikio yaliyoliwezesha kutambuliwa katika Hafla ya Kutunuku Tuzo za Utendaji Bora wa Taasisi za Umma iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam.

Akizungumza katika hafla hiyo, Msajili wa Hazina, Bw. Nehemia Mchechu, alisema TTCL imeonesha mafanikio makubwa kwa kubadili hasara ya Shilingi bilioni 18 iliyorekodiwa mwaka uliopita na kufikia faida ya Shilingi bilioni 22.9 katika mwaka huu wa fedha.

Alieleza kuwa mafanikio hayo yameiwezesha TTCL kutoa gawio la Shilingi bilioni 1.6 kwa Serikali, jambo linaloonesha kuwa uwekezaji wa Serikali katika mashirika ya umma unaendelea kuzaa matokeo chanya kupitia usimamizi madhubuti, ufanisi wa biashara na uwajibikaji.

Bw. Mchechu alisema ongezeko la gawio linalotolewa na taasisi za umma linaakisi mafanikio ya mageuzi ya kiutendaji na kimkakati yanayoendelea kutekelezwa chini ya Serikali ya Awamu ya Sita. Aliongeza kuwa taasisi za umma zina jukumu muhimu katika kuongeza mapato ya Serikali, kuchochea ukuaji wa uchumi na kuharakisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Akikabidhi tuzo hiyo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliipongeza TTCL kwa kurejea kwenye faida na kuanza kutoa gawio kwa Serikali, akieleza kuwa mafanikio hayo ni ushahidi wa kuimarika kwa uongozi, usimamizi wa rasilimali na ufanisi wa Shirika.

Mhe. Rais alisema taasisi za umma zinapaswa kuendelea kuongeza tija kwa kuwekeza katika teknolojia, ubunifu na mifumo ya kisasa ya usimamizi ili kuongeza ushindani, kuvutia uwekezaji na kutoa mchango mkubwa zaidi katika maendeleo ya uchumi wa Taifa.

Aidha, alizitaka taasisi za umma kuendelea kuzingatia uwajibikaji, matumizi bora ya rasilimali na utendaji unaozingatia matokeo, ili kuhakikisha uwekezaji wa Serikali unaleta manufaa endelevu kwa wananchi.

Mafanikio ya TTCL yanatokana na utekelezaji wa mageuzi ya kimkakati yaliyolenga kuimarisha utendaji wa biashara, kuongeza ufanisi wa huduma, kuboresha usimamizi wa rasilimali, kuwekeza katika teknolojia za kisasa na kujenga utamaduni wa uwajibikaji katika ngazi zote za Shirika.

Kutunukiwa Tuzo Maalum na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kunathibitisha hatua kubwa ambayo TTCL imepiga katika safari yake ya mabadiliko. Kurejea kwenye faida, kutoa gawio kwa Serikali na kuendelea kuboresha huduma kwa wananchi ni vielelezo vya dhamira ya Shirika ya kujenga kampuni ya mawasiliano yenye ushindani, endelevu na yenye mchango mkubwa katika maendeleo ya uchumi wa Taifa.

Mafanikio haya yanaendana na kaulimbiu ya mwaka huu, "Uwekezaji Wenye Matokeo ni Nguvu ya Uchumi Shindani na Maendeleo Endelevu kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050," na yanaifanya TTCL kuwa miongoni mwa taasisi za umma zinazoonesha matokeo halisi ya mageuzi ya kiutendaji na thamani ya uwekezaji wa Serikali kwa maendeleo ya Tanzania.