TTCL UWANJANI! WAFANYAKAZI WAJITOKEZA KULITANGAZA SHIRIKA KUPITIA SHIMMUTA 2026.
Na Adeline Berchimance
Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), kupitia Wafanyakazi wake, linashiriki katika Mashindano ya Michezo ya Mashirika, Taasisi na Makampuni (SHIMMUTA) 2026 yanayofanyika mkoani Morogoro kuanzia Novemba 6 hadi 21, 2026. Mashindano hayo yanayowakutanisha washiriki kutoka mashirika, taasisi na makampuni binafsi zaidi ya 100 yanafanyika chini ya kaulimbiu isemayo “Michezo ituunganishe kuelekea AFCON 2027”, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha mshikamano, umoja na maendeleo ya michezo nchini.
Ushiriki wa TTCL katika mashindano haya ni sehemu ya kuendelea kuimarisha utamaduni wa michezo ndani ya Shirika, huku ukiwapa Wafanyakazi fursa ya kuonesha vipaji vyao, uwezo wao na kulitangaza Shirika kupitia majukwaa ya michezo.
Aidha, ushiriki huu unaonesha dhamira ya TTCL katika kuunga mkono juhudi za kukuza michezo, kujenga mahusiano na taasisi nyingine pamoja na kuimarisha ushirikiano miongoni mwa wafanyakazi.
Hadi sasa, timu ya netiboli ya TTCL Queens imeshacheza jumla ya mechi nne dhidi ya timu za Chuo Kikuu Kishirikishi cha Elimu Dar es Salaam (DUCE), Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Chuo cha Ufundi Arusha ( ATC).
Mechi hizo zimekuwa sehemu ya kuonesha ushindani, nidhamu ya kimichezo na ari ya timu katika kuiwakilisha TTCL kwenye mashindano hayo.
Mbali na netiboli, TTCL inatarajia kushiriki katika michezo mbalimbali ya jadi na mingine itakayokuwa ikiendelea kadri ratiba ya mashindano itakavyoruhusu. Michezo hiyo inajumuisha karata, kurusha vishale (Darts) , mbio za riadha, drafti na michezo mingine ya jadi.
Ushiriki katika michezo hiyo unatoa zaidi kwa wafanyakazi wa TTCL kuonesha vipaji na uwezo wao katika maeneo mbalimbali ya michezo.
SHIMMUTA 2026 inajumuisha zaidi ya michezo 15, ikiwemo soka, netiboli, mpira wa kikapu, riadha, drafti, pool table na michezo ya jadi.
Wingi wa michezo na taasisi zinazoshiriki unatoa fursa ya kipekee ya kujenga mtandao wa mahusiano, kubadilishana uzoefu na kukuza mshikamano kati ya wafanyakazi wa sekta mbalimbali.
Ushiriki wa TTCL katika mashindano haya unakwenda sambamba na dhamira ya Shirika ya kutambua umuhimu wa ustawi wa wafanyakazi, afya bora, ushirikiano na kujenga mazingira yanayochochea utendaji wenye tija. Michezo ni nyenzo muhimu katika kukuza nidhamu, uwajibikaji, mshikamano na moyo wa kufanya kazi kwa pamoja, ambazo ni sifa muhimu pia katika kufanikisha malengo ya Shirika.