info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

TTCL SASA NI MWENDO WA “WALETEE” KUWARUDISHA WATANZANIA NYUMBANI

Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL Corporation) limezindua  Kampeni Mpya “WALETEE” kwa ajili ya wateja wa simu  ya Mkononi kujipatia vifurushi vya Dakika, SMS na Data ambavyo vimeboreshwa zaidi na kwa gharama nafuu. 

Akizungumza mapema leo Novemba 21,2024 jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo, Mkurugenzi wa Biashara wa TTCL, Vedastus Mwita, amesema kuwa lengo kuu la kampeni ya “WALETE” ni kuwafikia Watanzania wote na kutoa huduma zinazokidhi mahitaji yao ya mawasiliano, hasa katika nyakati hizi za teknolojia ya kidijitali.

“Kampeni ya WALETE ni sehemu ya kuwaeleza Watanzania wote kuwa mtandao wa TTCL wa simu ya mkononi hivi sasa unapatikana nchi nzima Tanzania bara na Zanzibar, mjini na vijijini. Popote Mtanzania alipo mawasiliano yetu yanapatikana kwa uhakika na gharama nafuu” amesema Bw. Mwita. 

Akizungumzia kuhusu vifurushi vinavyopatikana kwenye kampeni hii ya “WALETE”, Bw,Mwita amesema kuwa kifurushi cha Bufee Tena, kifurushi bora, gharama zake nafuu  na kimeboreshwa zaidi ili kumpa mteja uhakika wa mawasiliano. Kifurushi cha Bufee Tena  kinampa mteja uhuru wa kuchagua kiwango anachotaka, iwe Dakika, SMS, au Data, kulingana na mahitaji yake.

Aidha, kumefanyika maboresho kwa kuongeza BONASI kubwa kwenye vifurushi vya mawasiliano, ikiwemo Dakika, SMS kwenye Kifurushi cha Jiachie Xtraa, ambacho kinampa mteja fursa ya kupata muda wa kutosha wa kupiga kwenda mitandao yote na ujumbe mfupi (SMS) kwa gharama nafuu na bila ukomo wa muda.

Kupitia kifurushi kingine ni cha T-Connect Plus pia kimeboreshwa zaidi kwa mteja kupata intaneti na bonasi ya Dakika na SMS. 

Katika hatua nyingine, Mwita amesema kuwa kutokana na kukua kwa matumizi ya kidijitali, wameboresha upatikanaji wa vocha kwa njia ya kidijitali hivyo, hivi sasa mteja anaweza kupata vocha kupitia Mawakala wa T-RUSHA.

Aidha, vocha pia zinapatikana kwa njia ya kidijitali kupitia T-Pesa, kwenye Benki ya CRDB, NMB, Selcom, na mitandao mingine ya simu. Vilevile, vocha za kukwangua bado zinapatikana kwa mawakala waliopo maeneo mbalimbali na kwenye maduka yao.

Kwa upande wake, balozi wa kampeni ya “WALETE,” Clayton Chipando maarufu kama Baba Levo, ambaye pia ni Mtangazaji wa Wasafi FM na mwanamuziki, amesema kuwa TTCL kwenye upande wa Intaneti iko bora zaidi na ndipo inapoonesha ukubwa na ubora kwenye kumfanya Mtanzania kuperuzi kwa haraka zaidi.

“Mtandao wa TTCL kwenye upande wa Intaneti hapo ndipo tutakapoonyeshana ukubwa, kwani ndio wapo bora zaidi kwenye kumfanya Mtanzania kuperuzi kwa haraka zaidi,” alisema Baba Levo.

Amesema amewaita Watanzania  wote warejee nyumbani kwa kuwa hivi sasa kuna maboresho makubwa ambayo yamefanyika kwenye mtandao wetu, uhakika wa huduma na vifurushi vyenye gharama nafuu. 

 

.